1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afueni ya saa tatu kwa siku Aleppo kuingizwa misaada

Jane Nyingi11 Agosti 2016

Wizara ya ulinzi nchini Urusi imetangaza vikosi vyake vitasitisha kwa muda wa saa tatu kila siku harakati za kijeshi katika mji wa kaskazini mwa Syria wa Aleppo ili kuruhusu kuingizwa kwa misaada ya kiutu.

https://p.dw.com/p/1Jfqx
Sehemu ya mji unaodhibiwa na waasi Aleppo
Picha: Getty Images/AFP/K. Al-Masri

Luteni generali wa jeshi la Urusi Sergei Rudskoy hakuweka wazi ahueni hii itaendelea kwa siku ngapi. Punde baada ya tangazo hilo la Urusi, maafisa wakuu wanaosimamia kutolewa kwa misaada ya kiutu wa Umoja wa mataifa walisema muda huo wa saa tatu kwa siku hautoshi kuhakikisha wenyeji wanapata msaada wanaohitaji kwa dharura. Umoja huo ulikuwa umeomba mapigano hayo kusitishwa kwa muda wa saa 48 kwa wiki ili kuwezesha malori ya misaada kuingia Aleppo.

Syrien UN Rote Kreuz Zamalka
Malori ya misaada yakielekea miji ya Zamalka na Erbeen mashariki mwa Syria.Picha: picture-alliance/dpa/Syrian Arab Red Crescent

Katika mkutano na waandishi wa habari Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kutoa misaada ya kibinadamu Stephen O'Brien alisema karibu watu millioni mbili katika mji wa Aleppo hawana maji na hali huenda ikawa mbaya zaidi. Urusi ilikuwa imependekeza kuratibu shughuli hiyo ya utoaji misaada swala lilopingwa vikali na Umoja wa Mataifa."Ndio maana bila shaka tutajadili kwa umakini na kwa heshima na nchi yeyote mwanachama inayotoa mapendekezo,lakini mwisho, ni Umoja wa mataifa unaopaswa kusimamia upelekaji misaada, kwa mujibu wa kanuni zilizopo” alisema Stephen O'Brien

Syrien Krieg Kämpfe in Aleppo
Mapigano yachacha mji wa AllepoPicha: Getty Images/AFP/A. Alhalbi

Mapigano makali yamekua yakiendelea katika mji huo kati ya waasi na vikosi vya Syria vinavyoungwa mkono na Urusi huku pande zote mbili zikiimarisha mashambulizi.Hadi sasa haijawa wazi iwapo makundi ya waasi Syria pia yatasitisha mapigano katika muda uliokubaliwa wa saa tatu ili kuruhusu kuingia misaada Aleppo.

Madkatari Aleppo wa mwandikia barua Obama

Madaktari walio katika eneo linaloshikiliwa na waasi mashariki mwa mji wa Aleppo wameonya hali ni mbaya, huku wakisema wanakabiliwa na upungufu wa dawa na vifaa vya matibabu. Madaktari hao hata wamemwandikia barua Rais wa Marekani Barrack Obama kumtaka kuwasadia wenyeji wa Aleppo.

Shirika la kutetea haki za binadamu Syria limeripoti mapigano yanaendelea mjini humo hii leo licha ya Urusi kutangaza usitishwaji mapigano kwa saa kadhaa ili kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia mjini humo.

Mapigano ya hivi punde yalianza mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu baada ya vikosi vya serikali kukaribia kuidhibiti barabara ya Castelo, hii ikiwa barabara ya mwisho ya kuingia maeneo yanayoshikiliwa na waasi.

Mji wa Aleppo umegawanyika mara mbili huku waasi wakidhibiti eneo la mashariki na vikosi vya serikali vikisimamia eneo la magharibi tangu mapigano hayo kuanza mwaka 2012.

Mwandishi:Jane Nyingi/afp/dpa

Mhariri: Caro Robi