1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ahmad Khatami asema kuna njama dhidi ya Ayatollah Ali Khamenei

Kabogo Grace Patricia24 Julai 2009

Kiongozi huyo wa kidini ameyasema hayo leo baada ya Swala ya Ijumaa.

https://p.dw.com/p/IwuB
Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad (Shoto), akizungumza na Makamu mteule wa kwanza wa rais wa Iran, Esfandiar Rahim Mashaie, katika mkutano mjini Tehran, Iran.Picha: AP

Kiongozi wa kidini mwenye msimamo mkali nchini Iran, Ahmad Khatami, amesema kwamba kuna njama za kudhoofisha nafasi ya Kiongozi wa kidini wa ngazi ya juu, Ayatollah Ali Khamenei, baada ya uchaguzi wa mwezi uliopita uliogubikwa na hila. Kiongozi huyo ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waumini wa Kiislamu baada ya swala ya Ijumaa.

Khatami amesema kuna mikutano ya siri inayoendelea kupanga njama dhidi ya Ayatollah, lakini amesema kuwa wananchi wa Iran watamtetea kiongozi huyo hadi dakika ya mwisho. Ijumaa iliyopita, Akbar Hashemi Rafsanjani, rais wa zamani wa Iran, alisema kuwa nchi hiyo iko katika mzozo na kwamba kuna utata kuhusu matokeo ya uchaguzi. Shutuma hizo za Rafsanjani zimekuwa changamoto kwa uongozi wa Khamenei, kiongozi imara wa Iran, ambaye aliidhinisha ushindi wa Rais Mahmoud Ahmadinejad, mara baada ya uchaguzi.

Rais wa zamani wa Iran Mohammad Khatami na mgombea wa kiti cha urais aliyeshindwa katika uchaguzi huo, Mirhossein Mousavi, wamekataa matokeo ya uchaguzi huo, wakisema kuwa serikali ya Ahmadinejad iko madarakani kinyume cha sheria. Hatua ya Khamenei kuidhinisha ushindi wa Ahmadinejad ni tamko la mwisho la kuonyesha kuwa uchaguzi huo wa mwezi Juni, ulikuwa wa haki na huru.

Aidha, wakati wa sala ya Ijumaa, Khatami amerejea wito wake wa kumtaka Rais Ahmadinejad kumfukuza madarakani makamu wa kwanza wa rais aliyemteua wiki iliyopita. Rais Ahmadinejad alimteua Esfandiar Rahim Mashaie, hatua iliyozua gumzo kutokana na kauli yake ya kuiunga mkono Israel aliyoitoa mwaka uliopita. Baada ya viongozi hao wenye misimamo mikali kupinga uteuzi wa Esfandiar, mbunge wa ngazi ya juu wa Iran, wiki hii alisema kuwa dai la kufukuzwa kwa makamu mteule wa kwanza wa rais, limepelekwa kwa Rais Ahmadinejad.

Mbali na shinikizo hilo, Rais Ahmadinejad hajaonyesha dalili yoyote ya kumuondoa madarakani na badala yake amekuwa akimsifia Esfandiar kama mtu mwenye staha na aliyeonyesha uaminifu na uwajibikaji katika mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1976. Akisisitiza sifa zake, Rais Ahmadinejad amesema kuwa Esfandiar ni chaguo la Mungu, yuko msafi kama maji na muangavu kama kioo na kusema kuwa ni bahati mbaya watu wengi hawamfahamu vizuri.

Esfandiar Rahim Mashaie, ambaye mtoto wake wa kike ameolewa na mtoto wa Rais Ahmadinejad ni mtu asiyeogopa kusema ukweli, ambaye mwaka uliopita alisema kuwa Iran ni rafiki wa Israel.

Kufuatia uteuzi huo kundi la wanafunzi leo limeandamana katika mitaa ya mji wa Tehran, wakiwa wamebeba mabango yanayosema heshimu uongozi, huu ni msemo wa taifa, wakimtaka Rais Ahmadinejad kutengua uteuzi wake wa makamu wa kwanza wa rais.

Siyo tu Tehran ambako kuna maandamano ya kumpinga Rais Ahmadinejad, hapa Ujerumani pia katika miji ya Berlin na Mainz, kiasi cha raia 60 wa Iran ambao ni wafuasi wa upinzani, wamegoma kula kwa siku tatu, wakipinga ushindi wa Rais Ahmadinejad. Raia hao wanamtuhumu Rais Ahmadinejad kwa kuiba kura katika uchaguzi wa Juni 12, mwaka huu na kuendelea kwa vurugu dhidi ya waandamanaji mjini Tehran na katika miji mingine.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE/AFPE/DPAE)

Mhariri: Othman Miraji