1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ahmedinejad: aamuru kuongezwa kwa kiwango cha kurutubisha Uranium

7 Februari 2010

Jumuiya ya kimatifa yatoa jibu lake, baada ya kauli ya Ahmedinejad.

https://p.dw.com/p/Lv8G
Rais Mahmoud Ahmedinejad wa Iran, kuendelea na mpango wa nyuklia.Picha: AP

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua ya pamoja kuishinikiza serikali ya Iran kusitisha mradi wake wa nyuklia. Kauli ya Gates imekuja wakati Rais wa Iran Mahmoud Ahmedinejad ametoa amri kwa shirika la nishati ya atomiki la Iran kuanza kurutubisha madini ya Uranium kwa kiwango cha aslia mia 20. Waziri Gates akiwa mjini Roma, huko Italia, aliitolea wito jumuiya ya kimataifa kushirikiana katika suala la Iran.

Na kuhusu kauli ya Rais Ahmedinejad, Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Karl zu Guttenberg alisema jumuiya ya kimataifa inapaswa kuieleza Iran waziwazi kuwa subira yake imefikia mwisho.

Serikali ya Uingereza imesema mpango wa Iran wa kutaka kutengeneza nishati ya nyuklia ya kiwango cha juu, utakiuka maazimio matano ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Katika taarifa yake, wizara ya nchi za nje ya Uingereza ilisema, ripoti kutoka Iran kuwa inapanga kurutubisha nishati yake kwa kiwango cha asilia mia 20, ni jambo la kutia wasiwasi.

Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa Uingereza inatafakari hatua itakayochukua kwa kushirikiana na Shirika la kudhibiti Nishati ya Atomiki, IAEA na washirika wengine zikiwemo Ufaransa, Ujerumani, Marekani, Urusi na China.