1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ajali ya ndege Comoro ,bado hawajapatikana watu wengine walionusurika.

Sekione Kitojo1 Julai 2009

Hadi sasa hakuna maiti iliyopatikana kutoka katika ajali ya ndege ya Air Yemen iliyoanguka huko katika visiwa vya Comoro.

https://p.dw.com/p/Ierj
Jamaa wa abiria katika uwanja wa ndege wa Marseille kusini mwa Ufaransa jana Jumanne Julai 30, 2009 wakiulizia habari za jamaa zao.Picha: AP

Hadi sasa hakuna maiti iliyopatikana kutoka baharini baada ya ndege ya shirika la ndege la Yemen kuanguka , afisa mwandamizi wa serikali ya visiwa vya Comoro amesema leo, kinyume na taarifa za hapo awali kuwa miili ya watu watano imepatikana.


Jana Jumanne maafisa wa Comoro walisema kuwa maiti tano zilipatikana kutoka baharini ambako ndege chapa Airbus A 310 ilianguka ikiwa na abiria 153 . Ni mtu mmoja tu aliyenusurika hadi sasa, ambaye ni mtoto wac kike mwenye umri wa miaka 14, raia wa Ufaransa mwenye asili ya Comoro.

Katibu mkuu wa wizara ya usafirishaji nchini Comoro Abdillah Moigni, amesema leo kuwa wakati miili mitano ilionekana majini jana na juhudi zinafanywa ili kuwafikia , mawimbi makubwa baharini imezuwia wafanyakazi wa uokoaji kufanya hivyo.

Moja kati ya visanduku vyeusi, ambavyo ni vyombo vya kurekodia mawasiliano kati ya rubani na viwanja wa ndege kimefahamika kilipo na juhudi za kukipata zinaendelea. Ishara za kisanduku hicho zimepatikana jana usiku.

Kundi la waokoaji kutoka Ufaransa limejiunga na juhudi hizo za uokozi katika visiwa vya Comoro.

Wakati huo huo kundi la Wakomoro wenye hasira leo wamezuwia kuruka moja ya ndege katika uwanjani wa ndege wa Charles de Gaulle mjini Paris. Maandamano hayo yanafuatia kuanguka kwa ndege ya shirika la ndege la Yemen katika visiwa vya Comoro. Waandamanaji hao wanadai kuwa shirika hilo la ndege linatumia ndege zisizo salama katika njia kuelekea Comoro.

Wanatufanya kama mbwa, tunapofika Yemen wanatubadilishia ndege, wanatuingiza kama kwenye mapango.


Shirika hilo la ndege la Yemen limesisitiza leo kuwa lina sera imara kwa ajili ya ukarabati wa ndege zake na kupinga minong'ono kuwa tatizo la kiufundi ndio limesababisha kuanguka kwa ndege hiyo.

Waziri wa usafirishaji wa Ufaransa Dominique Bussereau amesema kuwa kulikuwa na matatizo katika ndege hii.

Kulikuwa na dosari kuhusiana na ndege hii na ukosefu wa hati za kibali cha usalama pamoja na ukosefu wa vifaa.

Ilikuwa ni katika mwaka 2007 ambapo tuliitaka Yemen Air kufanya marekebisho. Na kwa hali iliyokuwapo Ufaransa ilitoa rai hiyo na ilitumai ilizingatiwa. Nina wasi wasi haikuzingatiwa kwa sababu ndege hiyo haikufanya tena safari nchini Ufaransa.


Nae kamishna wa umoja wa Ulaya Antonio Tajani amesema mjini Brussels kuwa ndege kama ya shirika la ndege la Yemen haikustahili kuruka angani.

Kwa maoni yangu napaswa kupendekeza kuwa ndege kama hizi zinapaswa kuwekwa katika orodha ya ndege zilizopigwa marufuku kusafiri katika bara la Ulaya.


Wafanyakazi wa uwanja wa ndege walihamishia shughuli za kuruka ndege katika maeneo mengine ya uwanja huo na ndege hiyo ya Yemen iliruka ikiwa na abiria 100 ikielekea Marseille hadi katika mji mkuu wa Yemen Sana'a ikiwa ni njia ile ile iliyopitia ndege hiyo iliyoanguka.


Mwandishi Sekione Kitojo /AFPE/DPAE

Mhariri:Abdul-Rahman



►◄