1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege ya shirika la Yemen yaangukia bahari ya Hindi

Abdu Said Mtullya30 Juni 2009
https://p.dw.com/p/IeBY
Ndege ya abiria ya shirika la Yemen ilioangukia baharini Comoro.Picha: AP

Ndege ya  abiria ya shirika la Yemenia Air  imeangukia katika  bahari  ya Hindi karibu   na pwani ya kisiwa  cha  Comoro mapema  leo.

Watu  153  walikuwemo  mnamo ndege hiyo.Mtoto mmoja  amenusurika.

Ndege hiyo iliangukia  baharini  mapema asubuhi  leo kiasi  cha  robo saa  kabla ya  kuwasili  katika  kisiwa  cha  Moroni ambapo ilikuwa  inatarajiwa  kutua.    

Habari zinasema  baadhi  ya miili  ya watu  waliokufa katika  ajali  hiyo imeonekana.  Mashirika  ya habari yameripoti kuwa  mtu mmoja alienusuruka  ameokolewa.   Madakatari wamesema  kuwa mtu huyo   ni  mtoto. 

Hatahivyo juhudi  za uokoaji zinaendelea. Ufaransa  imepeleka manowari mbili na ndege moja  kutoka kwenye  kituo  chake cha karibu ili kuisaidia katika juhudi za uokaji.

 Ndege ya abiria ya shirika la Yemen aina   ya Airbus 310 ilikuwa  inatokea Sanaa mji mkuu  wa  Yemen  ikiwa  na abiria  142  na wafanyakazi 11. Ilianza safari  yake mjini Paris, Ufaransa  hapo jana  na  kutua  kwa  muda, katika miji ya Marseille,Djibouti na Sanaa.

Mpaka sasa  haijabainika kwa uhakika nini  hasa  kilisababisha ndege hiyo ianguke lakini maafisa  wanasema  hali ya hewa ilikuwa mbaya  wakati yalipotokea  maafa.

Ndege hiyo ilijaribu kutua, lakini ilishindikana. Baadae iligeuka na kupaa juu tena  na baada  ya hapo ilitoweka.


Mkurugenzi  wa uwanja  wa ndege  wa kimataifa wa Moroni Hadji Ali alisema hapo awali, kwamba kitengo  cha kufuatilia ndege kilipoteza  mawasiliano na ndege  hiyo ulipobakia muda mfupi kabla ya kutua.  

Hatahivyo habari kutoka Paris Ufaransa zinasema kuwa ndege  hiyo  ilikuwa inamulikwa  na  idara  ya usarifishaji  ya Ufaransa  kutokana  na  kugundulika hitilafu nyingi.

Maafisa wa Ufaransa  wameeleza kuwa kampuni ya ndege ya Yemen imekuwa inafuatiliwa  na idara za  Ufaransa na kwamba  ndege hiyo iliyoanguka,  hapo awali haikuwa  inaruka katika  anga ya Ufaransa kutokana na hitilafu.

Miongoni mwa abiria,  66 walikuwa wafaransa na  watoto  watatu wachanga. Lakini  idadi  kubwa walikuwa wananchi wa Comoro.




Mwandishi:Abdul-Mtullya/AFPE

Mhariri:M.Abdul-Rahman