1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika yatoa Matumaini

3 Oktoba 2014

Malengo ya Umoja wa Afrika hadi mwaka 2063,msimamo mpya wa Ujerumani kuelekea bara la Afrika na hali namna ilivyo katika nchi za Afrika Magharibi zinazoathirika kwa maradhi hatari ya Ebola magazetini

https://p.dw.com/p/1DPPE
Migodi Nchini MsumbijiPicha: DW/E. Silvestre

Tuanze na matumaini ya Umoja wa Afrika kwa bara la Afrika hadi ifikapo mwaka 2063.Jarida la "Kultur Austausch limeichambua ajenda 2063 iliyotungwa na mwenyekiti wa Umoja wa Afrika bibi Nkosozana Dlamini-Zuma na ambayo shabaha yake ni kuhakikisha katika kipindi cha miaka 50 inayokuja bara la Afrika litakuwa bara la amani na neema.Katika uchambuzi wake alioupa jina "Kujikwamua toka hali ya kuwa mhanga" mhariri wa jarida hilo anasema mtazamo huu ni matokeo ya juhudi zinazoendeshwa hivi sasa za mshikamano na maendeleo.Anajiuliza hata hivyo hatua gani zitapelekea kuligeuza bara la Afrika hadi mwaka 2063 liwe bara la amani na neema?Mwaka 2020 viongozi wa Afrika wanajiwekea matumaini ya kuunda Umoja wa kiuchumi utakaosaidia kuinua shughuli za kiuchumi kati ya nchi za kiafrika na kuinua ukuaji wa kiuchumi kutoka asili mia 14 hivi sasa na kufikia asili mia 50.Ufanisi wa miradi bunifu ya kilimo utasaidia kuitokomeza njaa barani Afrika na kuligeuza bara la Afrika kuwa bara linalosafirisha chakula kwa wingi duniani..Hata upande wa kisiasa mwaka 2020 unalengwa kuipatia Afrika amani na utulivu..Upande wa afya hadi mwaka 2020 homa ya Malaria itakuwa imetokomezwa na Ukimwi kudhibitiwa.Mhariri wa jarida la "Kultur Austauch anaungama ajenda 2063 inajibu kilio cha vijana walio wengi wa bara la Afrika,hata hivyo anajiuliza itatekelezwa kweli au itasalia karatasini tu?

Hata makampuni ya Ujerumani yana matumaini mema kwa Afrika

Gazeti la "masuala ya kiuchumi la Ujerumani "Handelsblatt" linazungumzia jinsi wnaviwanda wa Ujerumani wanavyoliangalia bara la Afrika hivi sasa."Wanaliangalia kuwa ni bara la matumaini badala ya "mashaka" licha ya Ebola na migogoro."Bara linalonyanyukia" ndio kichwa cha maneno cha ripoti ya gazeti hilo la mjini Düsseldorf.Mauwaji yanayofanywa na wanamgambo wa itikadi kali wa Boko Haram nchini Nigeria,janga la Ebola Afrika magharibi na picha za mashuwa zilizosheheni wakimbizi katika bahari ya Mediterenia hazikusaidia kupunguza matumaini yanayowekwa kwa bara la Afrika.Pato la ndani limeongezeka zaidi ya mara dufu katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita.Mataifa 48 ya kusini mwa jangwa la Sahara yanaweza kutegemea ukuaji wa wastani wa hadi asili mia sita.Zaidi ya hayo mataifa matano kati ya 10 ambayo uchumi wake unakuwa haraka,yanakutikana barani Afrika.Mhariri wa Handelsblatt anashadidia hoja zake kwanini wanaviwanda wa Ujerumani wanaliwekea matumaini makubwa bara la Afrika kwa kunukuu ripoti inayozungumzia faharasa za biashara kutoka ya benki kuu ya dunia inayosema ,kati ya mataifa 50 yanayoendeleza mageuzi ulimwenguni,18 yanakutikana Afrika.Mbali na mali ghafi na mishahara nafuu,makampuni ya Ujerumani yanawalenga zaidi wanunuzi wa bara hilo.Makampuni ya Ujerumani yanalenga zaidi kuimarisha shughuli zao Afrika Kusini,Nieria,Angola,Misri,Maroko na Kenya.

Ebola yavuruga mfumo wa maisha Liberia

Licha ya habari hizo za kutia moyo wahariri wa magazeti ya Ujerumani hawakulisahau janga linalotisha la maradhi ya Ebola katika Afrika magharibi.

Der Tagespiegel linazungzumhia jinsi maiti zilivyotapakaa na kusalia siku kadhaa majumbani nchini Liberia.Ebola imevuruga maisha ya watu na kudhoofisha shughuli za kiuchumi nchini Liberia ameandika mhariri wa gazeti hilo aliyezungumza na mwanaharakati wa haki za binaadam George Glaye.Kuenea haraka virusi vya maradhi ya Ebola kunaathiri mfumo mzima wa jamii-shule zimefungwa-shughuli za usafiri wa jamii zimepooza kwakua watu wanahofia kuambukizwa na kadalika.Kila idadi ya vifo inapoongozeka ndipo madhara ya kisaikolojia yanapozidi kuwa makubwa linaandika Der Tagesspiegel linalohisi serikali inashindwa kuidhibiti hali ya mambo ndio maana waliberia wanajiwekea matumani kutokana na mpango wa Marekani wa kutuma wanajeshi 3000 kusaidia kupambana na maradhi hayo hatari.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir.

Mhariri:Yusuf Saumu