1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin ajihami dhidi ya Ukraine

12 Agosti 2016

Rais wa Urusi, Vladmir Putin amekutana na baraza lake la usalama, siku moja baada ya Putin kuishutumu Ukraine kwa kuchochea mzozo kwenye eneo linalogombaniwa la Crimea, ambalo Urusi ililitwaa mwaka 2014.

https://p.dw.com/p/1Jh34
Sicherheitsrat Russland Wladimir Putin Moskau
Picha: Reuters/A. Druzhinin

Rais Putin alikutana na maafisa waandamizi wa kijeshi pamoja na maafisa wa kijasusi jana usiku na kutathmini upya hatua za kuchukua katika kupambana na ugaidi kwenye eneo la mpaka, bahari na eneo la anga la Crimea.

Rais Putin ameahidi kuchukua hatua madhubuti dhidi ya Ukraine, ambayo ameishutumu kwa kupanga mashambulizi ya kigaidi kwenye rasi ya Crimea, tuhuma ambazo zimekanushwa na Ukraine, ikiziita ni za uongo ambazo zinaonekana kama njama ya Urusi kutaka kueneza uhasama zaidi.

''Nadhani ni dhahiri kwamba maafisa wa Ukraine hawatafuti njia za kuyatatua matatizo haya kwa mazungumzo, bali kupitia vitendo vya kigaidi. Suala hili ni la kutisha sana,'' alisema Putin.

Hayo yanajiri wakati ambapo Wizara ya Ulinzi ya Urusi imetangaza kuwa kikosi cha jeshi la majini cha nchi hiyo, ambacho kimeweka kambi katika Bahari Nyeusi, Crimea, kitaanza kufanya mazoezi ya kivita kwenye eneo hilo katika kujibu mashambulizi ya kwenye maji yatakayofanywa na wahujumu.

Ukraine katika hali ya tahadhari

Rais wa Ukraine, Petro Poroshenko ameamuru kwamba vitengo vyote vya kijeshi karibu na Crimea na mashariki mwa Ukraine kuwekwa katika hali ya juu ya tahadhari, baada ya idara ya usalama ya Urusi kusema imefaulu kuyazima mashambulizi ya kigaidi ya jeshi la Ukraine katika Bahari Nyeusi wiki hii, shutuma ambazo zimekanushwa na serikali ya Ukraine.

Rais wa Ukraine, Petro Poroshenko
Rais wa Ukraine, Petro PoroshenkoPicha: picture-alliance/dpa/Anadolu Agency/H. Caliskan

Rais Poroshenko amesema anatafuta njia ya kufanya mazungumzo ya dharura na Rais Putin, pamoja na viongozi wa Ufaransa, Ujerumani, Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden na Rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk.

Wakati huo huo, Marekani imezitolea wito Ukraine na Urusi kujiepusha na malumbano kati yao na kuhimiza mazungumzo baina ya pande hizo mbili yaanze tena. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Elizabeth Trudeau, amesema nchi hiyo ina wasiwasi mkubwa na imezitaka nchi hizo kupunguza mvutano.

Aidha, Balozi wa Ukraine kwenye Umoja wa Mataifa, Volodymyr Yelchenko, amewaambia waandishi wa habari kwamba, katika kikao cha ndani cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Ukraine imeitaka Urusi kuonyesha ushahidi wa tuhuma dhidi yake kuhusu jaribio la mashambulizi ya kigaidi.

Katika mkutano huo uliofanyika kwa ombi maalum la Ukraine ili kuujadili mzozo kati yake na Urusi, Yelchenko, ameonya kuwa Urusi imepeleka zaidi ya wanajeshi 40,000 kwenye eneo la Crimea na kwamba hatua hiyo inaweza ikasababisha hali mbaya zaidi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/Reuters, AP, AFP
Mhariri: Mohammed Khelef