1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al-Burhan aridhia mazungumzo ya IGAD

Mohammed Khelef
27 Aprili 2023

Mkuu wa jeshi la Sudan, Jenerali Abdel-Fattah Al-Burhan, amekubali kutuma ujumbe wa wapatanishi katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, kuitikia wito wa mazungumzo uliotolewa na viongozi wa jumuiya ya IGAD.

https://p.dw.com/p/4QcTR
Kombobild Abdul Fattah Al-Burhan und Mohamed Hamdan Dagalo
Picha: Bandar Algaloud/Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Wakati Marekani na mataifa ya Kiafrika yakiwa yanawania kuongeza muda wa kusitisha mapigano nchini Sudan, ripoti kutoka mjini Khartoum zilisema mapambano yalikuwa yanaendelea kati ya wanajeshi wanaomtii mkuu wa majeshi, Jenerali Abdul-Fatteh al-Burhan, na wanamgambo wa kikosi cha dharura, RSF, kinachomtii Jenerali Mohamed Hamdani Dagalo. 

Taarifa iliyotolewa na kundi la RSF siku ya Alkhamis (Aprili 27) ililituhumu jeshi kwa kushambulia vikosi vya kundi hilo na kusambaza "uzushi", muda mfupi baada ya milio ya risasi kusikika kwenye viunga vya mji mkuu, Khartoum.

Soma zaidi: Sudan: Mkuu wa majeshi aashiria kulikubali pendekezo la IGAD la kuongeza muda wa kusitisha mapigano

Ndege za kijeshi zilionekana kwenye maeneo kadhaa ya nchi mapema ya siku hiyo.

Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyokuwa yakiendelea, yalitakiwa kumaliza muda wake usiku wa Alkhamis.

Ingawa mataifa ya kigeni yalijitahidi kukitumia kipindi cha masaa 72 kuwahamisha watu wao, shirika la habari la Reuters liliripoti kushuhudia raia wengi wa kigeni wakiendelea kunasa katikati ya mapigano hayo ya kuwania madaraka.

Jeshi kutuma wapatanishi Juba

Jioni ya Jumatano, jeshi lilisema kiongozi wake, Jenerali Al-Burhan, alikuwa ameridhia mpango wa kuongeza muda wa kusimamisha mapigano kwa masaa mengine 72 na kutuma ujumbe wa kijeshi katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, kwa mazungumzo ya kusaka amani.

Themenpaket - Sudan
Mkuu wa jeshi la Sudan, Jenerali Abdel-Fattah Burhan, amekubali pendekezo la kuongeza muda wa kusitisha mapigano.Picha: ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Soma zaidi: Mapigano yazuka upya nchini Sudan

Jeshi hilo liliongeza kuwa marais wa Sudan Kusini, Kenya, na Djibouti wanaowakilisha "Jumuiya ya Ushirikiano ya Pembe ya Afrika (IGAD) wamependekeza kuendelea kuongezwa muda kwa makubaliano ya sasa na wakati huo huo kukutana na pande hasimu kwa ajili ya mazungumzo."

Marekani, AU zasaka amani Sudan

Juhudi za IGAD zinakwenda sambamba na zile za Marekani zinazosimamiwa na waziri wake wa mambo ya kigeni, Anthony Blinken, ambaye alizungumza na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Muungano wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, juu ya nanma ya kumaliza vita nchini Sudan, ambako watu 512 wameshauawa na zaidi ya 4,000 kujeruhiwa tangu mapigano yaanza tarehe 15 Aprili. 

Sudan | Kämpfe in Khartoum
Moshi ukitanda mjini Khartoum kufuatia mapigano kati ya jeshi na wanamgambo.Picha: AFP/Getty Images

Mzozo huu umeongeza idadi ya wakimbizi wanaovuuka mpaka wa Sudan kuingia mataifa jirani, huku Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa likikisia kuwa watu 270,000 wanaweza kuwa wamekimbia Sudan Kusini na Chad.

Soma zaidi: Jeshi la Sudan lasema al-Bashir anashikiliwa hospitali ya kijeshi

Kutokana na matumizi ya ndege na makombora kushambuliana, pande zote mbili kwenye mzozo huu zinashutumiwa kuharibu majengo ya hospitali na makaazi ya raia, masoko na miundombinu ya kibiashara katika taifa ambalo robo ya watu wake milioni 46 walishakuwa wategemezi wa misaada ya kiutu.

Mbali na mji mkuu, Khartoum, mapigano yamesambaa hadi Darfur, ambako juzi na jana zilishuhudia vifo kadhaa vya raia, wizi wa mali na wasiwasi umeongezeka wa vita hivi kugeuka kuwa mapambano baina ya kikabila.

Vyanzo: Reuters, AFP