1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al Gore amepokea tuzo la amani la Nobel mjini Oslo leo

Josephat Charo10 Desemba 2007

Al Gore, na mwenyekiti wa jopo la Umoja wa Mataifa la mabadiliko ya hali ya hewa, Rajendra Pachauri, wamepokea tuzo la amani la Nobel hii leo mjini Oslo nchini Norway.

https://p.dw.com/p/CZpu
Al GorePicha: AP

Makamu wa zamani wa rais wa Marekani, Al Gore na mwanasayansi mkuu wa jopo la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia mabadiliko ya hali ya hewa, Rajendra Pachauri, wamekubali tuzo la amani la Nobel la mwaka huu wa 2007 kwa kuonya dhidi ya ongezeko la joto duniani na kuuhamasisha ulimwengu kuhusu njia za kukabiliana na tatizo hilo.

Tuzo hilo limetolewa na mwenyekiti wa kamati ya Nobel mjini Oslo nchini Norway, Ole Danbolt Mjos.

´Namuita mshindi wa tuzo la Nobel mwaka huu wa 2007, jopo la kimataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, likiwakilishwa na Rajerndra Pachauri, lije hapa mbele lipokee medali ya dhahabu na shahada ya diploma.´

´Namuita mshindi wa tuzo la Nobel mwaka huu wa 2007, Al Gore aje hapa mbele apokee medali ya dhahabu na shahada ya diploma.´

Ole Danbolt Mjos amesema Al Gore mwenye umri wa miaka 59, pamoja na jopo la kiserikali kuhusu mabadiliko ya hali hewa amesaidia kuweka misingi ya hatua zinazohitaji kuchukuliwa kukabiliana na ongezeko la joto duniani.

Katika hotuba yake wakati wa sherehe ya utoaji wa tuzo hilo katika ukumbi wa mjini Oslo, Mjos amesema uamuzi wa kamati hiyo haukuwa mgumu kwa kuwa maswala yanayohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa ndiyo yanayopewa kipaumbele katika siasa kwa wakati huu.

Mjos amesema mtazamo uliochukuliwa na jopo la Umoja wa Mataifa lililoundwa mnamo mwaka wa 1988 likiwa na wanasayansi 2,500 na uchunguzi wa mabadiliko ya hali ya hewa unaoendelea unaweza kutumika katika nyanja nyingine kama vile viumbe mbalimbali duniani, kuenea kwa jangwa na uvuvi usio mipaka katika bahari. Amemtaja Al Gore kama mtu pekee aliyefanya mengi kuweka msingi wa hatua za kisiasa zitakazochukuliwa dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Mjos ameonya kwa kusema, ´Kupuuzia changamoto za ongezeko la joto duniani kunaweza kuwa uhalifu. Bila shaka ni kutomtii Mungu! Ni dhambi! Hali ya baadaye ya sayari yetu hii nzuri iko mikononi mwetu. Sisi ni wasimamizi wa vitu vyote vilivyoumbwa na Mungu.´

Katika hotuba yake ya kulikubali tuzo la amani la Nobel, Al Gore, akizungumzia mabadiliko ya hali ya hewa amesema ulimwengu una homa ya mafua inayozidi. Aidha amesema vitendo vya binadamu vinalinganiswha na vita dhidi ya dunia na kuongeza kuwa wakati umewadia kufanya mkataba wa amani na sayari yetu.

Al Gore ambaye anatarajiwa baadaye wiki hii kwenda katika kisiwa cha Bali nchini Indonesia kuhudhuria mkutano kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, amezitaka Marekani na China zichukue hatua za haraka kupunguza gesi za viwandani la sivyo zibakie katika vitabu vya historia kwa kushindwa kuchukua hatua.

Mwenyekiti wa jopo la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia mabadiliko ya hali ya hewa, Rajendra Pachauri, amesema tuzo la amani la Nobel linatambua umuhimu wa jukumu la elimu katika uundaji wa sera. Amezitaja athari za mazingira katika nyanja mbalimbali zikiwemo usalama wa chakula, afya na tatizo la kuyafikia maji safi.

´Kwa ujumla athari za mabadiliko ya hali ya hewa zinazozikabili baadhi ya jamii maskini zaidi duniani huenda isiwezekane kukabiliana nazo. Baadhi ya jamii huenda ziendelee kukabiliwa na athari hizo na huenda hali ya kiuchumi ikashuka, kipato kupotea na kushindwa kumudu maisha.´

Pachauri amesisiti kwamba ipo haja ya kuongeza kasi ya kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.

´Nadhani tunalazimika kutumia ushawishi wetu kuuambia ulimwengu kwamba hatujafanya mengi. Ukiangalia ongezeko la kiwango cha gesi za viwandani tangu mkataba wa Kyoto uliposainiwa linadhihirisha matokeo mabaya.´

Tuzo za Nobel za sayansi ya dawa, fizikia, kemia na uchumi zinatarajiwa kutolewa kwa washindi baadaye leo mjini Stockholm Sweden. Mshindi wa tuzo la Nobel la uandishi, Doris Lessing, ameshindwa kuhudhuria sherehe hiyo na ataipokea zawadi yake mjini London Uingereza.