1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al Gore ana wasiwasi kuhusu mkutano wa Bali

Josephat Charo12 Desemba 2007

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ameutolea mwito mkutano wa Bali ufikie makubaliano.

https://p.dw.com/p/CakR
Makamu wa zamani wa rais wa Marekani Al GorePicha: AP

Washindi wa tunzo ya amani ya Nobel, makamu wa zamani wa rais nchini Markani, Al Gore, na kiongozi wa jopo la Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, Rajendra Pachauri, wameeleza wasiwasi wao kuhusu mazungumzo ya mkutano unaojadili mabadiliko ya hewa kisiwani Bali nchini Indonesia. Mkutano huo unakabiliwa na changamoto kubwa huku India ikizitaka nchi tajiri duniani ziongoze juhudi za kupunguza gesi chafu za viwandani.

Al Gore na Rajendra Pachauri wamesema baadhi ya ripoti kutoka Bali Indonesia zinatia wasiwasi lakini wakasema wana mataumaini makubaliano yatafikiwa. Al Gore amesema kutokana na uzoefu katika mikutano mingine kama hiyo makubaliano hufikiwa katika muda wa saa 48 za mwisho kabla mkutano kumalizika, na hata mara nyingine katika muda wa saa nne na nane za mwisho.

Rajendra Pachauri amesema kufikia sasa hakuna ufanisi wowote uliopatikana katika siku chache zilizopita kwenye mkutano wa Bali. Ameongeza kusema kuwa angependelea makubaliano yafikiwe katika síku mbili au tatu zijazo akionya hakuna wakati wa kuchezea kuhusiana na swala zima la ongezeko la joto dunaini.

Wajumbe kutoka nchi zaidi ya 180 wanaokutana katika kisiwa cha mapumziko cha Bali nchini Indonesia wanatakiwa kufikia keshokutwa Ijumaa wakubaliane juu ya mfumo wa kukabiliana na ongezeko ya joto duniani wakati mkataba wa Kyoto utakapomalizika ifikapo mwaka wa 2012.

Akizungumza wakati alipoyafungua mazungumzo ya kiwizara katika mkutano wa Bali, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, alilisitiza haja ya kufikia makubaliano.

´Ikiwa tutaondoka Bali bila kufikia makubaliano hatutakuwa tumewavunja mioyo viongozi wetu tu, bali pia hata wale wanaotutegemea sisi kutafuta suluhisho, yaani wakaazi wote ulimwenguni.´

Aidha Ban Ki Moon alisema watu wote duniani ni sehemu ya tatizo la ongezeko la joto.

´Sisi sote ni sehemu ya tatizo zima la ongezeko la joto duniani. Hebu sote tuwe sehemu ya suluhisho linaloanzia Bali. Tulibadili tatizo kubwa la mabadiliko ya hali ya hewa kuwa makubaliano kuhusu kuilinda hali ya hewa.´

Mawaziri wanalazimika waamue ikiwa mashauriano yamalizike kwenye mkutano utakaofanyika mjini Copenhagen nchini Denmark mwishoni mwa mwaka wa 2009. Umoja wa Mataifa unasema muda hadi mwaka wa 2009 utazipa nchi wakati wa kuidhinisha mkataba mpya utakaofikiwa ili uweze kutekelzwa mwishoni mwa mwaka wa 2012 wakati mkataba wa Kyoto utakapomalizika.

Kuwepo kwa muda wowote kati ya mikataba hiyo miwili huenda kukaathiri sana viwango vya gesi ya carbon dioxide kwa mujibu wa viwango vilivyoweka katika mkataba ya Kyoto. Baadhi ya nchi lakini zinataka kusiwe na tarehe maalumu zikiwa na matumaini kwamba rais mpya wa Marekani anayetarajiwa kuchukua madaraka Januari mwaka 2009, ataiongoza Marekani kusaini mkataba wa Kyoto.

Rais wa Indonesia Susilo Bambang Yudhyono amesema, ´Lazima tuhakikishe kwamba Marekani kama dola kuu la kiuchumi duniani, mtoaji mkubwa wa gesi chafu za viwandani na nchi inayoongoza katika teknolojia duniani, ni sehemu ya mpango utakaotumika baada ya mwaka wa 2012.´

Umoja wa Ulaya unazitaka nchi zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani zifikrie kupunguza utoaji wa gesi za viwandani kwa asilimia kati ya 25 na 40 kufikia mwaka wa 2020 ikilinganishwa na viwango vya mwaka wa 1990. Umoja huo unasema hii itadhihirisha kwamba nchi tajiri zinataka kweli kufanya mashauriano, lakini Marekani, Japan, Canada, Australia na nchi nyengine zinapinga. Hata hiyo waziri mkuu wa Australia, Kevin Ruud, amesema serikali yake imejitolea kupunguza gesi chafu za viwandani.

´Serikali imejitolea kwa dhati kupunguza utoaji wa gesi chafu kwa asilimia 60 ifikapo mwaka wa 2050 ikilinganishwa na viwango vya mwaka wa 2000. Australia itatekeleza mpango wa kupunguza gesi za viwandani kufikia mwaka wa 2010 kufikia viwango hivi. Tutaongeza viwango vya nishati endelevu kwa asilimia 20 ya kiwango cha kitaifa cha umeme kufikia mwaka wa 2020.´

Ukataji ovyo wa miti na kubadilishana teknolojia ni maswala muhimu kwa nchi zinazoendelea. Tatizo katika taarifa ya pamoja inayotarajiwa kutolewa baada ya mkutano wa Bali ni vipi kuzilipa fidia nchi maskini zinazohifadhi misitu yao na jinsi ya kuhimiza mabadilishano ya tekonolojia safi kutoka nchi tajiri hadi mataifa maskini. Yote haya yatajulikana mkutanao utakapomalizika Ijumaa ijayo.