1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al shabaab waua katika mgahawa Mogadishu

26 Agosti 2016

Watu saba wameuwawa na wengine 20 kuokolewa katika mashambulizi yaliyofanywa na wapiganaji wa kundi la al- Shabaab katika mgahawa maarufu kwa vijana na maafisa wa serikali ufukweni mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

https://p.dw.com/p/1Jq97
Askari nchini Somalia akiwa eneo ambalo kumewahi kutokea mlipuko wa bomu la kutegwa kwenye gariPicha: picture-alliance/AP Photo/F. Abdi Warsameh

Idadi hiyo inajumuisha raia, maafisa wa polisi na wapiganaji wawili wa kundi hilo, ambapo mwanamgambo mmoja anashikiliwa na polisi.

Ripoti zinasema washambuliaji waliuvamia mkahawa huo kwa kutumia gari lililosheheni mabomu, kabla ya kuingia ndani na kuwarushia watu risasi ovyo ovyo usiku wa jana (Alhamis ya 25 Agosti). Kisha kuaanza majibizano ya risasi na vikosi vya usalama, huku washambuliaji wakirusha mabomu ya mkono kwa maafisa wa usalama waliokuwa wakilinda eneo hilo.

Katika waraka uliotolewa kupitia mtandao wa kutuma ujumbe mfupi wa Telegram, kundi la al-Shabaab limekiri kuhusika na mashambulizi hayo ambayo yalifanyika saa 9:00 alfariji kwa majira ya Somalia, huku wakidai kuwa wameua watu wengi zaidi.

Akizumgumza kwa niaba ya serikali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mogadishu, Kanali Abshir Bishaar, ameviambia vyombo vya habari kuwa vikosi vya usalama vimewadhibiti washambuliaji na mkahawa huo sasa upo katika ulinzi mkali wa askari wa serikali ya Somalia.

Somalia Selbstmordanschlag auf Nasahablood Hotel in Mogadischu
Askari wakiwa na silaha nje ya eneo la hoteli ambalo limewahi kushambuliwa kwa bomuPicha: Reuters/F. Omar

Taarifa zinasema kuwa al-Shabaab wameelekeza mashambulizi katika mkahawa huo kwa sababu unatambulika kwa kuwa na watu ambao wanapingana na maadili ya dini ya Kiislamu na kujihusisha na vitendo haramu, kwa mujibu wa tafsiri yao ya dini.

Hatari ya nchi nyingine za Afrika kushambuliwa

Hii ni mara ya pili mwaka huu kwa kundi hilo kufanya mashambulizi katika eneo la ufukweni huko Lido na katika maeneo mengine ya sehemu za kuuza chakula na katika maduka ya kuuza bidhaa mbalimbali ambayo ni ya wafanyabiashara maarufu na Wasomali waliokuwa wakiishi nje ya nchi hiyo. Mwishoni mwa mwezi Januari, walitegesha bomu eneo la Libo na kuua watu 20.

Kundi hilo linajiimarisha tena upya baada ya kurejeshwa nyuma zana na majeshi ya Umoja wa Afrika nchini humo (AMISOM) na kampeni yake ya sasa inatajwa kulenga kuvuruga taratibu za kufanyika kwa uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufayika mwezi Septemba na Oktoba mwaka huu.

Kundi hilo limekuwa likiupinga utawala wa serikali ya Somalia ambayo inaungwa mkono na mataifa mengine duniani, wakati wao wakitaka nchi hiyo yenye takribani 99% ya Waislamu iongozwe kwa kufuata sheria za dini hiyo.

Kundi hilo pia limekuwa likifanya mashambulizi katika nchi nyingine za jirani kama vile Kenya na Uganda na hivi karibuni kumetolewa onyo huenda wakafanya mashambulizi katika nchi za Ethiopia, Djibouti na Tanzania.

Mwandishi: Celina Mwakabwale/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef