1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al Shabab imewaua watu 147 nchini Kenya

3 Aprili 2015

Takriban watu 147 wameuwawa na wengine 70 kujeruhiwa Alhamisi (02.04.2015) wakati watu wenye silaha walipovamia kitivo cha chuo kikuu karibu na mpaka wa Kenya na Somalia na kuwashikilia mateka wanafunzi kadhaa.

https://p.dw.com/p/1F1nI
Kenia Attentat in Garissa
Picha: picture-alliance/AP Photo

Kulikuwa na majibizano ya risasi yaliodumu kwa masaa kadhaa kati ya watu hao na vikosi vya usalama.Mkuu wa jeshi la polisi nchini Kenya Joseph Bonet amesema katika taarifa polisi na wanajeshi wamezingira na kukifunga Chuo Kikuu cha Garissa na wamekuwa wakijaribu kuwatimuwa kwenye chuo hicho watu hao wenye silaha.

Amesema wavamizi hao walikuwa wakifyetuwa risasi ovyo ndani ya jengo la chuo hicho.Polisi aliekuwweko kwenye eneo la tukio hilo amekaririwa akisema baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakishikiliwa mateka lakini hakutaja wangapi ila amesema ni wengi.

Mwanafunzi mmoja aliyeweza kutoroka katika chuo hicho amesema walivamiwa wakati wakiwa usingizini na kwamba ameshuhudia wanaume watano waliojifunika nyuso zao wakiwa na silaha nzito.

Al Shabab ladai kuhusika

Kundi la al Shabab limedai kuhusika na shambulio hilo ambapo msemaji wa operesheni za kijeshi wa kundi hilo Sheikh Abdiasis Abu Musab amekaririwa akisema kwamba waliwapambanuwa watu waliokuwa wakiwashikilia na kuwachilia huru wale walio Waislamu.

Wanafunzi wakitoka kwenye nyumba walikojihifadhi baada ya chuo chao kuvamiwa Garissa.(02.03.2015)
Polisi ya Ken ya nje ya jengo la chuo kikuu Garissa.(02.04.2015)Picha: picture-alliance/AP Photo

Ameliambia shirika la habari la Uingereza kwamba kuna miili mingi ya Wakristo waliouwawa ndani ya jengo hilo na wanawashikilia Wakristo wengi wakiwa hai na kwamba mapambano bado yanaendelea ndani ya chuo hicho.

Kundi la wanamgambo wa Kiislamu wa itikadi kali nchini Somalia la al Shabab ambalo lina mafungamano na kundi la Al Qaeda huko nyuma lilifanya mashambulizi huko Garissa ambayo iko kama kilomita 200 kutoka mpaka wa Somalia na sehemu nyengine za Kenya.

Majeraha ya risasi

Kwa muijibu wa taarifa iliyotolewa kwenye mtandao wa Twitter na Kituo cha Taifa cha Operesheni za Majanga watu wengi waliojeruhiwa walikuwa wamepata majeraha ya risasi na wanne kati yao hali yao ni mahtuti ambapo wamepelekwa Nairobi kwa matibabu.Inaelezwa kwamba watu sitini wamejeruhiwa,

Jeshi la Kenya likikizingira Chuo Kikuu cha Garissa. (02.04.2015)
Jeshi la Kenya likikizingira Chuo Kikuu cha Garissa. (02.04.2015)Picha: Reuters

Grace Kai mwanafunzi katika Chuo cha Mafunzo ya Walimu kilioko jirani na Garissa amesema kulikuwa na onyo kwamba kutakuwepo na shambulio.Ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba baadhi ya wageni walionekana katika mji wa Garissa na wanatuhumiwa kuwa magaidi.

Amesema waliambiwa na mwalimu wao mkuu hapo Jumatatu kwamba kulikuwa na watu wenye sura za kigeni walionekana katika chuo chao ambapo Jumanne waliruhusiwa kurudi nyumbani na chuo chao kufungwa lakini kitivo hicho cha chuo kikuu kiliendelea kuwa wazi na sasa kimeshambuliwa.

Al Shabab kundi ambalo limehusika na shambulio lililosababisha maafa hapo mwaka 2013 katika jengo la maduka la Westgate katika kitongoji cha kifahari mjini Nairobi limetangaza litaiadhibu Kenya kwa kutuma wanajeshi wake nchini Somalia kwa aili ya kupambana bega kwa bega na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika dhidi ya kundi hilo.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AP/AFP

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman