1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sheria ya kuwaadhibu magaidi yapitishwa Misri

Mjahida17 Agosti 2015

Vyombo vya habari vya serikali ya Misri vimesema rais Abdel-Fattah el-Sissi ameidhinisha sheria mpya ya kupambana na ugaidi iliokosolewa na baadhi ya wanasiasa na mashirika ya kutetea haki za binaadamu.

https://p.dw.com/p/1GGav
Rais Abdel Fattah al-Sisi
Rais Abdel Fattah al-SisiPicha: Reuters/The Egyptian Presidency

Sheria hiyo iliyopitishwa hapo jana na kuchapishwa katika gazeti la serikali inachambua ugaidi kwa undani zaidi, kwa kuuelezea kuwa kitendo chochote kinachoharibu amani kwa kutumia nguvu.

Adhabu kali imo pia katika sheria hiyo kwa uhalifu tofauti ikiwemo kupigia debe au kuunga mkono kwa aina yoyote kosa lolote la kigaidi pamoja na kuharibu majengo ya serikali na miundo mbinu.

Sheria hiyo inatoa faini kubwa ya dola 25,000 kwa wanahabari watakaokuwa wamechapisha habari au taarifa za uongo juu ya visa vya ugaidi, au habari zitakazokuwa zimekwenda kinyume na maelezo au ripoti za wizara ya ulinzi nchini humo.

Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi
Rais wa Misri Abdel Fattah al-SisiPicha: Getty Images/Afp/K. Desouki

Waandishi habari hao pia huenda wakawachishwa kazi kwa kuandika taarifa zisizoeleweka kama inavyosema sheria hiyo ya kupambana na ugaidi. Misri haijawahi kuwa na bunge kwa zaidi ya miaka miwili na mamlaka yote ya bunge yanafanywa na rais el-Sissi. Majadiliano yoyote yanafanyika kupitia vyombo husika vya habari au kwa mikutano ya faragha.

Rais huyo wa Misri Abdul Fata asl sisi alikuwa ameahidi kuweka sheria kali ya kupambana na ugaidi itakayohakikisha magaidi wanakabiliwa na mkono wa sheria haraka iwezekanavyo baada ya kuuwawa kwa mwendesha mashtaka mkuu nchini humo Hisham Barakat mwezi Juni, mwaka huu.

Waandishi habari, wasema sheria haijazingatia uhuru wao

Hata hivyo kamati ya waandishi habari ya misri iliyo na makao yake makuu mjini Newyork Marekani, imelaani vikali sheria hiyo iliyosema haizingatii uhuru wa vyombo vya habari na inakiuka katiba ya Misri.

Misri imekuwa ikikumbwa na wimbi kubwa la wapiganaji wa jihadi wanaoaminika kuwa na mafungamano na kundi la dola la kiislamu katika rasi ya Sinai, eneo linalopakana na Israel na eneo la Palestina la Ukanda wa Gaza.

Hali hiyo imejitokeza tangu Al sisi alipomuondoa madarakani rais Mohammed Morsi mwezi Julai mwaka 2013, wakati huo akiwa mkuu wa jeshi.

Wafuasi wa chama cha udugu wa kiislamu kilichotangazwa kuwa kundi la kigaidi
Wafuasi wa chama cha udugu wa kiislamu kilichotangazwa kuwa kundi la kigaidiPicha: Mohamed El-Shaed/AFP/Getty Images

Serikali ya Misri pia ililitangaza kundi la udugu wa kiislamu wanaomuunga mkono Mohammed Morsi kuwa kundi la Kigaidi na kuwatia nguvuni maelfu ya wanachama wake, wakiwashutumu kusababisha ghasia baada ya kuondolewa Mohammed Morsi.

Uchaguzi wa bunge ulitarajiwa kufanyika mapema mwaka 2014 chini ya mkakati uliowekwa na rais wa mpito wakati huo Adly Mansour, baada ya kuondolewa kwa rais Mursi lakini hilo halikufanyika na hadi sasa uchaguzi huo unaendelea kuahirishwa.

Muandishi Amina Abubakar /AP/AFP/dpa

Mhariri: Iddi Ssessanga