1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Alan Johnston aachiwa huru

4 Julai 2007

Muandishi habari wa Idhaa ya BBC ya Uingereza aliachwa leo huru na watekanyara huko Gaza na yuko njiani kurudi nyumbani Uingereza baada ya kuwa kizuizini kwa miezi 4.

https://p.dw.com/p/CB35
Alan Johnston huru
Alan Johnston huruPicha: AP

Baada ya kiasi cha miezi 4 kizuizini,ripota wa Idhaa ya BBC Alan Johnston ameachwa huru mapema hii leo na kikundi chenye siasa kali cha wapalestina.Akifuatana na wajumbe wa kibalozi wa Uingereza alivuka mpaka wa mwambao wa gaza mapema asubuhi ya leo na kuingia Jeruselem.

Muandishi habari wa Idhaa ya BBC Alan Johston aliachwa huru hii leo kufuatia majadiliano yaliofanywa kati ya ukoo wa kipalestina na waziri-mkuu wa zamani wa chama cha Hamas, Ismail Haniyeh,alietangaza pia atapigania kuachwa huru kwa yule mwanajeshi wa Israel, Gilad Schalit alienyakuliwa kiasi cha mwaka ummoja uliopita.

Johnston, amekuwa kizuizini tangu Machi 12.Akiwa huru tena alisema na ninamnukulu,

“yafurahisha mno kuwa nje.”

Akiongeza alisema zaidi:

“Miezi 16 iliopita, ndio kipindi kibaya kabisa maishani mwangu.Ilikua hali ngumu kwangu kutengwa na ulimwengu wa nje na ni hali ya kutisha kuangukia mikononi mwa watu dhaifu kabisa bila kujua lini kisa hiki kitamalizika.Baada ya miezi 2, unaanza kuwaza iwapo bado kuna miezi 8 au 18 utabaki kifungoni na naamini habusu yeyote anajiuliza swali hili na anajitahidi kubaki katika afya njema.”

Alan Johnston alisema kuachwa huru ni kuvuta mno pumzi ambako huwezi kufikiria.Akakishukuru chama cha Hamas kwa kumuokoa pamoja na wale wote waliochangia uhuru wake.

Aliwaeleza waliomteka kuwa ni majambazi na watu hatari kabisa ambao huwezi kujua watakufania nini.Walitishia kumaliza maisha yake mara kwa mara kwa mbinu tofauti.Hatahivyo, alisema hakutumiliwa nguvu,lakini kuna nyakati akibughudhiwa na akawaita waliomteka “watovu wa adabu”.

Johnston akaongeza:

“Lazima niwaambie kuwa watekanyara wakijiaamini sana hadi wiki chache zilizopita pale ilipodhihirika kwamba chama cha Hamas kimechukua dhamana ya usalama kamili katika Gaza.hapo tena watekanyara waliingiwa mno na wasi wasi na nikaanza kuhisi labda mwisho wangu umefika.”

Johston alifichua kwamba mara 2 alipatwa na maradhi wakati wa kifungo chake cha miezi 4.

Alan alisema alikuwa na radio wakati akiwa kifungoni na aliweza kusikiliza visa vilivyokuwa vikipita mwambao wa gaza pamoja na juhudi zilizokuwa zikifanywa kumkomboa kupitia idhaa ya BBC.

Alisema akiota mara nyingi kuwa huru.Kwani, alisema ilikuwa taabu kuamini siku moja sitaamka usingizini na kutoka hayi chumba hicho nilichokuwamo.

Tangu kushika hatamu kamili za mwambao wa Gaza, chama cha Hamas kiliimarisha juhudi za kumkomboa Alan Johnston, kikiwa na shauku ya kubainisha kuwa kina uwezo na mamlaka ya kusimamia sheria na n idhamu katika mwambao huo.

Usiku wa kuamkia leo,vikosi vya Hamas vililizingira eneo la mwambao wa Gaza ambako Jeshi Islam-kikundi kilicho na mafungamano na ukoo wa Doghmush una shina lake na ambako ikidhaniwa Johnston alifichwa.

Chini ya shinikizo na hofu kuwa vikosi hivyo vya Hamas huenda vikajaribu kumkomboa Johnston kwa nguvu ,Jeshi Islam lilichapisha video ikimuonesha Johnston amevalishwa kizbao chenye miripuko ya mabomu ambamo alionya kuwa watekanyara wake wametishia kuyafyatua endapo Hamas ikihujumu pale alipo.

Akiwa amekuwa kifungoni kwa kiasi cha siku 114,Johnston mwenye umri wa miaka 45,amekuwa kifumngoni kitambo zaidi kuliko raia yeyote yule wa kigeni aliechukuliwea mateka katika mwambao wa Gaza.

Akiwa njiani sasa kurejea nyumbani Uingereza,baba yake Johnston alisema amezungumza nae kwa simu kwa ufupi. Mama yake Margaret na baba yake Graham Johnston,walisema wamefurahishwa ajabu kabisa kuona jiinamizi limepita.