1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Algeria yakataa kuwa ngazi katika kundi C

Sekione Kitojo19 Juni 2010

Timu ya Algeria moja kati ya timu tano wawakilishi wa bara la Afrika imepigana kiume jana Ijumaa na kutoka sare ya bila kufungana na Uingereza katika mchezo wao wa pili wa kundi C.

https://p.dw.com/p/NxDu
Asamoah Gyan wa Ghana akishangilia bao dhidi ya Slovenia. Ghana inapambana na Australia leo .Picha: AP

Uingereza isiyokuwa na meno, kibogoyo, ndivyo inavyoelezwa timu ya taifa ya Uingereza na waandishi wengi wa habari katika fainali za mwaka huu za kombe la dunia zinazofanyika kwa mara ya kwanza katika bara la Afrika nchini Afrika kusini. Timu ya taifa ya Uingereza ilifanikiwa tu kutoka sare ya bila kufungana na Algeria, moja ya timu inayowakilisha bara la Afrika , na kuweka matumaini yake ya kubakia katika kinyang'anyiro hicho cha kombe la dunia katika mzani wakati Serbia iliipiga mweleka Ujerumani iliyocheza na wachezaji kumi uwanjani, kwa bao 1-0 , baada ya Miro Klose kutolewa kwa kadi nyekundu.

Kikosi cha Fabio Capello, cha Simba wa Uingereza, ambacho tayari kimo katika mbinyo baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Marekani, US Boys katika mchezo wa ufunguzi wa kundi lao la C, ilihangaika kutafuta njia kuwashinda Algeria na kuwapa wakosoaji wao silaha zaidi baada ya kucheza tena chini ya kiwango.

Ikipigiwa upatu kuwa moja kati ya timu zinazoweza kutoroka na kombe la dunia mwaka huu, Uingereza hivi sasa inahitaji kuwashinda viongozi wa kundi hilo la C Slovenia katika mchezo wao wa mwisho siku ya Jumatano mjini Port Elizabeth ili kuwa na uhakika wa kufika duru ya pili. Fabio Capello hakuweza kupata maneno ya kuelezea ni kwa nini timu yake iliyofanikiwa kuingia katika fainali hizi kwa mbembe imeshindwa kupata njia ya kutamba huko Afrika kusini. Tulipoteza pasi nyingi, mipira mingi. Haukuwa mchezo mzuri. Tunahitaji kufanya vizuri zaidi, amesema Capello.

Leo hii mchana ni zamu ya wawakilishi wengine wa bara la Afrika , Ghana na Cameroon. Ghana inatumai kuinua bendera ya matumaini ya Afrika juu, katika fainali hizi za kwanza kufanyika katika bara la Afrika, katika mashindano ambayo yanatia hamasa kwa mafanikio ya timu zenye uzito mdogo dhidi ya zile zinazotajika kuwa vigogo.Ghana bila shaka itapata mashabiki wengi, mjini Rustenburg leo mchana wakati Black Stars watakapojaribu kuikabili Australia, ambayo imejeruhiwa na Ujerumani kwa mabao 4-0 katika mchezo wa ufunguzi.

Vigogo wengine wa Afrika Cameroon , walianza kwa kusua sua baada ya kuangushwa kwa bao 1-0 na Japan katika mchezo wao wa ufunguzi katika kundi E. Cameroon wanataka kuzika fedheha hiyo leo Jumamosi mjini Pretoria dhidi ya Denmark.

Mchezo mwingine siku ya leo Jumamosi pia unahusu timu za kundi E, ambapo Uholanzi inapambana na Japan wakitumai kufanya vizuri zaidi kutoka mchezo wao usioridhisha hata baada ya kushinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Denmark. Wadachi watamkosa winga wao hatari Arjen Robben, licha ya kuwa hata bila ya Robben uwezo wao wa kushambulia ni mkubwa.

Mwandishi: Sekione Kitojo / RTRE/AFPE