1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Aliyeamuru mashambulizi Mali akiri makosa ICC

22 Agosti 2016

Katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), kiongozi wa kikundi cha Waislamu wenye msimamo mkali nchini Mali, Ahmad al-Faqi, amekiri kuhusika na mashambulizi yaliyosababisha uharibifu eneo la turathi za Dunia.

https://p.dw.com/p/1JmkH
Eneo lililoshambuliwa katika mji wa Timbuktu nchini MaliPicha: picture-alliance/AP Photo/B. Ahmed

Akiwa amevalia suti nyeusi, mpiganaji huyo wa itikadi kali amekiri kuhusika kuamuru kufanyika kwa shambulio katika eneo la makuburi ya wanazuoni yanayotukuzwa pamoja na msikiti katika mji wa Timbuktu ambao ulitumika kama kituo cha mafunzo ya Kiislam kati karne ya 15 na 16. Wapiganaji wa itikadi kali wanaamini kuwa kutukuza wanazuoni wa zamani ni kufuru.

Mbali na kukiri kuhusika na kosa hilo, amewaomba Waislamu duniani kote kutojihusisha na vitendo vya aina hiyo kwani havina faida yoyote kibinadamu.

Mali Ahmad Al Faqi Al Mahdi vor dem Internationalen Strafgerichtshof in Den Haag
Ahmad al-Faqi kiongozi wa kikundi cha waislam wenye msimamo mkali aliyekiri kuhusikaPicha: Reuters/R. van Lonkhuisen

Kesi hiyo iliyofunguliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) inaelezwa kuwa ni kesi ya aina yake na inatazamiwa kuwa fundisho kwa watu na makundi mengine yenye kuharibu sehemu za kihistoria na utamaduni kwamba vitendo vyao havitanyamaziwa.

Iran Bokovo, mkurugezi wa UNESCO, anasema uharibifu wa maeneo yanayotambulika kama turathi za dunia imekuwa mbinu ya kivita ambayo inatumika kueneza hofu na chuki katika mizozo iliyoko sasa duniani.

Timbuktu mji wa watakatifu 333

Mji wa Timbuktu ulijengwa kati ya karne ya tano na 12 na watu wa kabila la Tuareg na unafahamika kama mji wa watakatifu 333 kwa kuwa na idadi kubwa ya wanazuoni wa Kiislamu waliozikwa hapo.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda, anasema kwa mara ya kwanza mahakama ya ICC inasikiliza kesi kama hii.

“Hii ni mara ya kwanza mahakama kutambua umuhimu na kushiriki katika vita kinyume na kila aina ya uharibifu kwa kuwa vitendo kama hivyo ni chanzo cha uharibifu dhidi ya binadamu.”

Mtaalamu wa masuala ya sheria, Mariana Pena katika Chuo Kikuu Huria cha Justice Initiative, anasema kwa upande mmoja anapongeza kesi kama hii kupewa kipaumbele lakini kwa upande pili anasema amevunjwa moyo kuona makosa mengine hayakufunguliwa mashitaka.

Hukumu ya kesi hiyo inatarajiwa kutolewa hivi karibuni baada ya kusikilizwa kwa siku tano ambapo hukumu ya juu inaweza kuwa kifungo cha miaka 30 jela, japo hukumu ya al-Mahdi inaweza kupungua na kufungwa miaka 9 mpaka 12.

Mwandishi: Celina Mwakabwale/AFP/DPA

Mhariri: Mohammed Khelef