1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Aliyekuwa makamu wa rais wa Catalonia kusalia gerezani

5 Januari 2018

Mahakama Kuu ya Uhispania iliamuru kutomwachilia makamu wa zamani wa Rais wa jimbo la Catalonia Oriol Junqueras, baada ya miezi miwili jela.

https://p.dw.com/p/2qPWO
Spanien Katalonien Oriol Junqueras
Picha: Reuters/J. Barbancho

Haya yanajiri wakati mamlaka zikichunguza kuhusika kwake kwenye harakati ya kuunga mkono uhuru wa Catalonia kujitenga na Uhispania.

Katika uamuzi huo, majaji walisema kuna hatari kwamba Junqueras angeweza tena kufanya uhalifu kwa sababu hakuonyesha dalili za kutaka kubadilisha mienendo yake. Anazuliwa kwa tuhuma za uasi, uchochezi na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Junqueras  alikuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha hatua ya kutaka kujitenga na Uhispania kupitia kura ya maoni ambayo ilifanyika mnamo Oktoba 1 licha ya marufuku ya mahakama.

Baada ya kura hiyo, Uhispania iliwatimua maafisa wa serikali ya jimbo la Catalonia ikiwa ni pamoja na Junqueras, ikavunja utawala wa ndani wa jimbo hilo, bunge lake na kuitisha uchaguzi wa mapema.

Uchaguzi wa Desemba 21 uliwapa wanaotaka kujitenga wingi mdogo katika bunge la jimbo na ilikuwa pigo kwa Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy, ambaye alikuwa na matumaini ya kuondoa vuguvugu linalopigia debe uhuru wa Catalonia na kutatua mgogoro mkubwa wa kisiasa nchini Hispania kwa miongo kadhaa.

Uamuzi wa mahakama utamzuia Junqueras kuapishwa katika kikao cha ufunguzi wa bunge la Catalonia mwezi Januari 17 na kukwamisha juhudi ya vyama vinavotaka kujitenga ya kutafuta kiongozi ambaye hajafungwa gerezani au kukimbilia nje ya nchi.

Rais wa zamani wa Catalonia Carles Puigdemont aliyeko uhamishoni Ubelgiji
Rais wa zamani wa Catalonia Carles Puigdemont aliyeko uhamishoni UbelgijiPicha: Reuters/E. Vidal

Chama cha mrengo wa kushoto cha Junqueras cha Esquerra Republicana  kiliibuka kama chama cha pili kikubwa cha wanaotaka kujitenga, viti vichache nyuma ya chama cha Rais wa zamani wa Catalonia Carles Puigdemont's cha Junts per Catalunya yaani umoja wa Catalonia.

Chama kinachofuata sera za masoko na kinachopendelea Umoja wa Uhispania, Ciudadanos, yaani raia, kilipata viti vingi zaidi, lakini vyama vyengine vinavyunga mkono pia Umoja wa taifa hilo, havikupata viti vya kutosha kuweza kupata wingi bungeni na kuunda serikali.

Puigdemont anabaki uhamishoni mjini Brussels, ingawa amesema atarudi Catalonia kama serikali ya Hispania ingempa ahadi ya kutomkamata. Baada ya hukumu ya Mahakama Kuu, Puigdemont alielezea kwenye mtandao wa Twitter: "Kuna mgogoro kati ya Catalonia na Hispania ambayo inapaswa kutatuliwa.

Wanasheria wa chama cha Esquerra wamesema Puigdemont ana haki tena awe rais wa Catalonia, lakini ikiwa hawezi kurudi kutoka Brussels anapaswa kumpisha Junqueras kwa nafasi hiyo.
 

Mwandishi: Fathiya Omar/RTRE

Mhariri: Gakuba, Daniel