1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Aliyeteuliwa na Trump kuwa mshauri wa usalama, akataa

17 Februari 2017

Mtu aliyeteuliwa na rais Donald Trump kulijaza pengo la mshauri wa kitaifa wa usalama Robert Haward ameikataa kazi hiyo. Trump alilazimika kumtafuta atakayeichukua nafasi hiyo kufuatia kujiuzulu kwa Michael Flynn. 

https://p.dw.com/p/2Xkgp
USA PK Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: picture alliance/AP Photo/P. Martinez Monsivais

Katika taarifa Haward ambaye ni mwanajeshi mstaafu, amesema kwamba kwa sasa hawezi kujitolea kuyatimiza mahitaji ya kazi hiyo.

"Tangu kustaafu kwangu, nina fursa sasa ya kuangazia masuala ya kifedha na ya kifamilia sasa na iwapo nitaichukua nafasi hii, basi itakuwa ni changamoto kuyatimiza," alisema Haward katika taarifa kwa shirika la habari la CNN.

Lakini mwendani wa Haward ameiambia CNN kwamba aliikataa nafasi hiyo kutokana na hali ya kutoeleweka katika utawala wa Marekani kwa sasa. Duru karibu na rais Trump, ililiambia gazeti la Washington Post kwamba, uamuzi wa Haward ulifanywa pia kutokana na kuwa hakuwa na uhakika iwapo angekua na uwezo wa kuchagua wafanyakazi wake mwenyewe.

Trump amekataa kuwasiliana na urusi wakati wa kampeni

Kuondoka kwa Flynn mapema juma hili kumelifanya baraza la kitaifa la usalama nchini Marekani liwe katika hali tete, huku ikiripotiwa kwamba utawala wa Trump unapata wakati mgumu kuteua watu kujaza takriban nafasi 60 kati ya 200 za kazi zilizopo.

USA Michael Flynn
Michael Flynn alijiuzulu wiki iliyopitaPicha: Reuters/C. Barria

Huku hayo yakiarifiwa, rais Trump amekanusha kwamba yeye na maafisa wake wa kampeni waliwasiliana na maafisa wa Urusi kabla uchaguzi wa mwaka jana nchini Marekani.

Rais huyo mpya ambaye amekabiliwa na msukosuko wiki hii kuhusiana na madai hayo ya kuwasiliana na Urusi, alizungumza katika mkutano na waandishi wa habari huko Washington na amesema kwamba taarifa zozote zinazomuhusisha na Urusi ni za uongo mtupu.

Trump kutoa marufuku nyengine ya kuingia Marekani wiki ijayo

"Naweza kuwaambia kwamba similiki chochote nchini Urusi, sina madeni nchini Urusi, sina biashara zozote nchini urusi. Rais Putin alinipigia kunipongeza kwa ushindi wangu wa uchaguzi, kisha akanipigia tena kwa kunipongeza baada ya kuapishwa, na lilikuwa ni jambo zuri. Lakini viongozi wengine pia kutoka mataifa mengine walinipigia. hivyo ndivyo ilivyokuwa, habari za Urusi ni porojo tu, hizi ni porojo tu zinazoenezwa na vyombo vya habari," alisema Trump.

Russland Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Getty Images/AFP/S. Karpukhin

Katika mkutano huo na waandishi wa habari pia, Trump aliitetea ajenda yake ya kisiasa akisema kwamba wiki ijayo atatoa marufuku nyengine ya kuingia Marekani iliyofanyiwa marekebisho. Marufuku yake ya kwanza ilikosolewa sana, na mahakama nchini humo ikaisimamisha.

Amesema pia kwamba Marekani itaweka mikataba mipya ya kibiashara itakayozuia mataifa mengine kuitumia nchi yake kujinufaisha. Trump lakini amesema kuwa hatofanya ukatili katika kukabiliana na suala la wahamiaji wasio na vibali na ambao waliingia nchini humo kama watoto, na ambao kwa sasa wanalindwa kisheria dhidi ya kurejeshwa makwao.

Mwandishi: Jacob Safari/AFP/DPA

Mhariri: Daniel Gakuba