1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AMMAN : Vikosi vya Iraq kuongoza shughuli za usalama Juni 2007

1 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCnp

Waziri Mkuu wa Iraq Nuri al Maliki amesema vikosi vya serikali yake vitakuwa na uwezo wa kuchukua madaraka ya usalama kutoka kwa vikosi vya Marekani ifikapo mwezi wa Juni mwaka 2007 hatua ambayo inaweza kuviwezesha vikosi vya Marekani kuanza kuondoka nchini humo.

Katika mkutano wa viongozi mjini Amman Jordan Rais George W. Bush wa Marekani amesisitiza kwamba vikosi vya Marekani vitaendelea kubakia nchini Iraq kwa kadri vitakavyohitajiwa na serikali ya Iraq.

Mazungumzo yamefanyika wakati mauaji ya kimadhehebu yakizidi kupamba moto nchini kote Iraq ambapo maiti za wahanga 49 waliouwawa zimepatikana katika kipindi cha masaa 24 na jeshi la Marekani limesema mwanajeshi wake mmoja ameuwawa katika mapigano na kufanya idadi ya wanajeshi wake waliouwawa mwezi wa Novemba kupindukia 70.

Wakati huo huo waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeir ameanza ziara ya siku nne Mashariki ya Kati ikiwa ni maandalizi ya Ujerumani kushika wadhifa wa Umoja wa Ulaya kuanzia mwezi wa Januari mwakani.

Kituo chake cha kwanza kitakuwa Jordan ambapo leo hii kunafanyika mkutano wa kila mwaka wa mawaziri wa mambo ya nje wa Kundi la Mataifa Manane yenye Maendeleo Makubwa ya Viwanda Duniani,mataifa ya Mashariki ya Kati na yale ya Afrika.