1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty International yatoa ripoti yake juu ya Mali

MjahidA1 Februari 2013

Shirika la Amnesty International limesema raia wa Mali wanakabiliwa na hatari kutoka kila upande kutokana na ghasia zinazoendelea nchini humo, ikiwa ni pamoja na vitendo vya uvunjaji wa haki za binaadamu

https://p.dw.com/p/17WEX
Nembo ya shirika la Amnesty International
Nembo ya shirika la Amnesty International

Kulingana na mtafiti wa shirika hilo la Kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International Gaetan Mootoo, kuna ushahidi wa kutosha unaoonesha jeshi la Mali lilitekeleza mauaji ya kusudi kwa raia wake.

Mootoo alikuwa kwenye taifa hilo la Afrika Magharibi kufanya utafiti juu ya ghasia zinazoendelea huko.

Ripoti yake inasema waasi wa kaskazini mwa Mali pia wamefanya uvunjifu mkubwa wa haki za binaadamu, kwa kuwaua raia na hata kutumia wataoto katika mapambano. Shirika hilo linasema hatua hiyo moja kwa moja inavunja sheria ya kimataifa ya haki za binaadamu.

Mwanajeshi wa Mali akishauriana na mwenzake wa Ufaransa
Mwanajeshi wa Mali akishauriana na mwenzake wa UfaransaPicha: Reuters

Katika mji wa Diabaly, watu waliohojiwa na Amnesty International, wamesema walishuhudia watoto waliokuwa na umri wa miaka 10 tu, wakibeba bunduki na kutembea pamoja na waasi.

Mjini Segou nako, shirika hilo lilipata nafasi ya kuwahoji watoto wawili wanaotumika katika kundi hilo na mmoja wao alionesha dalili ya kurukwa na akili.

Huku hayo yakiarifiwa kuna ushahidi katika ripoti hiyo unaoonesha kuwa raia watano wakiweno watoto watatu waliuwawa katika mashambulizi ya angani yaliyofanywa na jeshi la Mali pamoja na lile la Ufaransa katika operesheni ya pamoja ya kuwaondoa waasi kaskazini mwa Mali.

Waasi wa Mali
Waasi wa MaliPicha: Reuters

"Mapigano yakiendelea nchini Mali kila upande unapaswa uzingatie na kuheshimu haki za binaadamu ili raia wa kawaida wasiumizwe na kuhusishwa katika ghasia," alisema Mootoo.

Kutokana na mashahidi waliozungumza na shirika hilo la Amnesyt International, wakati vikosi vya Ufaransa vilipoingia nchini humo kupambana na waasi mnamo tarehe 10 Januari, jeshi la Mali liliwatia mbaroni na kuwauwa zaidi ya watu 20 kaskazini mwa Mali.

Baadhi ya wakaazi wa Mali
Baadhi ya wakaazi wa MaliPicha: AP

Walioshuhudia kisa hicho walielezea namna jeshi hilo lilivyokuwa likitupa miili katika mto mmoja uliokuwa karibu, wanajeshi hao pia walisemekana kuipiga risasi miili hiyo baada ya kuitupa majini. Serikali ya Mali imekuwa ikilenga watu wanaodhaniwa kuwa na mafungamano na waasi, wengi wao wakiwa na asili za Kiarabu na Kituareg.

Shirika hilo limesema kutumiwa kwa watoto katika jeshi na waasi ni lazima ukomeshwe mara moja na pia kutaka jeshi la Mali na lile la Ufaransa wanaopambana na waasi wa kaskazini mwa Mali kuzingatia na kuheshimu haki za binaadamu wakati wa mapambanao hayo.

Mwandishi: Amina Abubakar/Amnesty International

Mhariri: Mohammed Khelef