1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ANC yapata pigo katika uchaguzi

7 Agosti 2016

Chama tawala nchini Afrika kusini The African National Congress , ANC, kimepoteza nguvu zake katika uchaguzi wa serikali za mitaa katika eneo la Tshwane, eneo lililoko katika mji mkuu wa Afrika kusini Pretoria

https://p.dw.com/p/1Jcri
Südafrika Kommunalwahlen
Mwanamke akipiga kura yake Afrika kusiniPicha: picture-alliance/AP Photo/D. Farrell

Matokeo ya janaJumamosi (06.08.2016) yalionesha chama cha upinzani cha Democratic Alliance , DA kikipata ushindi mkubwa kikishika nafasi ya pili katika uchaguzi ambao chama cha ANC kimefanya vibaya tangu kumalizika kwa enzi za ubaguzi wa rangi.

Wahlen Südafrika Mmusi Maimane
Kiongozi wa chama cha Democratic Alliance nchini Afrika kusini Mmusi MaimanePicha: picture-alliance/AP Photo/H. Verwey

Matokeo ya uchaguzi uliofanyika siku ya Jumatano umebadilisha uwanda wa kisiasa nchini Afrika kusini, ambako chama cha ANC kimetawala kwa karibu bila kupingwa tangu kilipofikisha mwisho utawala wa Wazungu wachache mwaka 1994, kikiongozwa na Nelson Mandela.

Ukosefu wa ajira, uchumi uliokwama na kashfa zinazomzunguka rais Jacob Zuma zimesababisha wapiga kura kukiadhibu chama cha ANC, na kubadilisha muonekano wa uchaguzi mkuu wa taifa mwaka 2019 na kuwahamasisha kwa kiasi kikubwa wapinzani wa Zuma ndani ya chama cha ANC kuweza kupambana nae.

Symbolbild Wahlen Südafrika
Mpiga kura wa chama cha kikomunist SACP akionesha furaha yake nchini Afrika kusiniPicha: Getty Images/AFP/R. Jantilal

Eneo la viwanda

Kwa kulinda hadhi yake, chama cha ANC kilishinda jimbo la mji wa Johannesburg, mji ambao ni ngome kuu ya kibiashara na kifedha , kikipata asilimia 45 ya kura dhidi ya asilimia 38 ilizopata chama cha DA, lakini kitahitajika kuunda serikali ya mseto kuweza kutawala jimbo hilo.

Ushindi katika eneo la Tshwane na Nelson Mandela Bay , maeneo ambayo yanajumuisha kitovu cha viwanda kwa ajili ya mji wa Port Elizabeth , ni ushindi wa kishindo kwa chama cha DA, ambacho pia kilipata udhibiti wa mji wa Cape Town, mji ambao kimeudhibiti tangu mwaka 2006.

Südafrika Kommunalwahlen
Mwanamke akipiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa nchini Afrika kusiniPicha: Getty Images/AFP/G. Guercia

Mwaka jana kilimchagua kiongozi wake wa kwanza mweusi, Mmusi Maimane, wakati kikijaribu kujitoa kutoka katika taswira ya chama ambacho kinalinda maslahi tu ya wazungu.

"Inatoa ishara kwa kila mtu kwamba wimbi katika nchi yetu linabadilika," Maimane aliwaambia waandishi habari jana Jumamosi,(06.08.2016).

ANC kimeshinda kura nyingi

Chama cha ANC bado kimeshinda kura nyingi kwa jumla, na kinafanya kazi kuunda muungano katika miji mbali mbali ambako kimeshindwa kupata wingi wa kutosha.

Südafrika Kommunalwahlen
Upigaji kura katika uchaguzi wa serikali za mitaaPicha: picture-alliance/AP Photo

"Tumo katika majadiliano wakati huu tunapozungumza," alisema Paul Mashatile mwenyekiti wa chama cha ANC katika jimbo la Gauteng, ambalo ni pamoja na Tshwane na Johannesburg.

"Ni wazi kwamba watu wetu, waungaji wetu mkono wa asili, bado wako nasi lakini huenda sio watu wengi waliojitokeza kupiga kura kwa hiyo tunahitaji kwenda na kujua kwa nini."

Südafrika Wahlen Wahlkampagne
Mkutano wa hadhara wa chama cha Economic Freedom Fighters nchini Afrika kusiniPicha: Getty Images/AFP/M. Safodien

Chama cha DA pia kitahitaji kuunda muungano ili kuweza kutawala katika maeneo ya Tshwane na Nelson mandela Bay.

Katika matamshi yake ya kwanza kwa umma tangu matokeo ya uchaguzi yatolewe, rais Jacob Zuma alisema Afrika kusini ni "democrasia ambako tofauti za maoni ya kisiasa na tofauti za kisiasa zinaruhusiwa kunawiri".

Chama cha ANC kimepoteza uungwaji mkono miongoni mwa wapiga kura ambao wanahisi maisha yao hayajabadilika, na upinzani umemshutumu rais Zuma kwa kuharibu uchumi. Mamilioni ya wapiga kura wa mijini sasa wanaangalia mbali zaidi ya sifa ya chama hicho ya ukombozi na kuangalia zaidi kuhusiana na uchumi ambao umevurugika ukiwa katika ukingo wa kuingia katika mdororo.

Südafrika Johannesburg Oppoosition EFF Julius Malema
Kiongizi wa chama cha EFF Julius MalemaPicha: picture-alliance/dpa/C. Tukiri

Zuma aliwatia hofu wawekezaji mwezi Desemba kwa kubadilisha mawaziri wa fedha mara mbili katika muda wa wiki moja, na kusababisha sarafu ya rand kuporomoka. Sarafu hiyo imeanza kupanda tangu wakati huo na ilipata msukumo kutokana na kutokuwapo na ghasia wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre

Mhariri: Isaac Gamba