1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ANKARA:Abullah Gul ajitoa kwenye kinyang'anyiro cha mgombea urais

6 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CC4I

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Abdullah Gul amejiondoa kwenye kinyang’anyiro cha kugombea kiti cha urais baada ya bunge kushindwa kwa mara nyingine kupata idadi ya wabunge wanaohitajika kupiga kura ya kumchagua mgombea wa uarais. Bunge limeshindwa kuwapata wabunge 367 kuweza kupiga kura hiyo. Duru ya mwanzo ya uchaguzi wa mgombea urais bungeni ilibatilishwa na mahakama ya kikatiba wiki iliyopita kutokana na sababu kama hii ya kukosekana wabunge wakutosha kuhalalisha zoezi hilo.

Vyama vya upinzani hii leo vilikataa kushiriki kikao cha bunge wakipinga kuchaguliwa kwa Abdullah Gul kuwa mgombea pekee wa chama tawala cha AK.

Kabla ya kikao hicho cha leo Abdullah Gul alisema kwamba atajiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho ikiwa chama chake cha AK kitashindwa kupata uungaji mkono Bungeni.

Mamia kwa maelfu ya watu waliandamana hapo jana katika miji ya magharibi mwa Uturuki kuunga mkono siasa zitenganishwe na dini.

Maandamano hayo yalifanyika kwenye miji ya Manisa na Canakkale.

Waandamanaji wamepinga kuchaguliwa kwa bwana Gul kuwa mgombea wa kiti cha Urais kwa kuhofia kwamba akichaguliwa ataanzisha utawala wa sheria za kiislamu nchini Uturuki.