1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Annan aonya Syria kutumbukia vitani

Admin.WagnerD8 Juni 2012

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya nchi za Kiarabu katika mzozo wa Syria Koffi Annan, ameonya kuwa zisipochukuliwa hatua kuushinikiza utawala nchini humo, hali itazidi kuwa mbaya.

https://p.dw.com/p/15Ab8
Koffi Annan akizungumza mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Koffi Annan akizungumza mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: picture alliance / ZUMAPRESS.com

Akiongea katika hali ya kukataa tamaa, Annan alirejea wito wake kwa mataifa makubwa kumuonya Assad juu ya madhara yatakayotokana na kushindwa kwake kuheshimu mpango wa amani wa hatua sita.

"Ukiukaji unaendelea, nchi inazidi kukingamia na kuwa ya itikadi kali. Kama mambo hayatabadilika, mustakabali unaelekea kuwa wa ukandamizaji wa kikatili, mauaji ya kimbari, vurugu za kidini na mwishowe tutashuhudia vita vikubwa vya wenyewe kwa wenywe," alisema Annan.

Annan aliliambia Baraza la Usalama kuwa ipo haja ya kuwepo na shinikizo la pamoja na lenye nguvu kwa Assad na kuongeza kuwa matokeo laazima yaonekane haraka vinginevyo mgogoro huu utashindwa kudhibitiwa. Alionya kuwa kadiri jamii ya kimataifa inavyozidi kusubiri, ndivyo mustakabali wa Syria unavyozidi kuwa wa kiza.

Katibu Mkuu Ban Ki-Moon akizungumza mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ilivyo nchini Syria.
Katibu Mkuu Ban Ki-Moon akizungumza mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ilivyo nchini Syria.Picha: dapd

"Laazima tubuni njia na uwanja sawa wa kuchukua hatua, na tuchukuwe hatua kama mmoja. Hatua za mtu mmoja moja au Uingiliaji wa taifa moja moja hautaleta sulugu ya Mgogoro," aliongeza Annan.

Ban Ki-Moon naye aonya
Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alisema baada ya mkutano huo kuwa kuna uwezekano mkubwa wa Syria kutoka kwenye ncha ya vita ya kutumbukia kabisaa vitani na kuongeza kuwa hivis sasa dalili zote zinaonyesha nchi hiyo inanyemelewa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vyenye madhara makubwa si tu kwa Syria bali kwa kanda nzima.

Ki-Moon alisema watu wa Syria, wanavuja damu, wana njaa na wanachotaka hivi sasa ni amani na heshima. Na juu ya yote, wanataka kuona jamii ya kimataifa ikichukua hatua. Alisema hakuna anayeweza kutabiri hali itakuwaje huko Syria, kwa hivyo laazima jamii ya kimataifa ijiandae kwa lolote lile. "Laazima tuwe tayari kuitikia hali zozote zinazoweza kutokea," alitahadharisha Ki-Moon.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likijadili hali nchini Syria.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likijadili hali nchini Syria.Picha: dapd

Mkutano huu ulifanyika saa chache baada ya kuripotiwa kwa mauaji mengine ya kutisha ya watu 80 katika kijiji cha Al-Kubeir ambapo waangalizi wa amani wa Umoja wa Mataifa walirushiwa risasi wakati wanajaribu kuingia kijijini humo kuthibitisha taarifa za mauaji hayo. Siku ya Ijumaa timu hiyo ya waangalizi ilikuwa inafanya juhudi nyingine kujaribu kuingia kijijini humo.

Annan ataka kuishirikisha Iran katika usuluhishi
Annan alisema alikuwa katika mandalizi ya kuunda kundi la kujadili mgogoro wa Syria na alitarajia kuwa Iran ingekuwa moja wa washiriki katika kundi hilo lakini Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa alipinga kushirikishwa kwa irani aliyoiita mharibifu na kuongeza kuwa hadi sasa Iran haijaonyesha utayari wake katika kuchangia urejeshwaji wa amani nchini Syria.

Wakati huo huo, habari kutoka Syria zinasema ndege za serikali zinaendelea kuushambulia vikali mji wa Khalidiya uliopo kati kati ya Mkoa wa Homs katika kile kinachoonekana kama mandalizi ya vikosi kuuvamia upya mji huo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFPE\APE\
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman