1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Annan kutua Kenya kwa ajili ya upatanishi.

14 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CpR4

Nairobi. Pande zinazopingana nchini Kenya zinajitayarisha leo kwa ajili ya mapambano mapya bungeni hapo kesho pamoja na mitaani licha ya juhudi mpya za kimataifa kufanya upatanishi kuhusiana na mzozo wa uchaguzi ambao umesababisha watu 612 hadi sasa kuuwawa.

Lakini kwa watu wengi katika taifa hilo la Afrika mashariki, umuhimu mkubwa ni kuwawezesha mamilioni ya wanafunzi kurejea shuleni baada ya kucheleweshwa kwa muda wa wiki moja kutokana na ghasia zilizosababishwa na kuchaguliwa tena kwa rais Mwai Kibaki hapo Desemba 27.

Mzozo huo umechafua jina la Kenya katika demokrasia pamoja na uchumi ambao ni imara, na kusababisha upungufu wa bidhaa kwa mataifa jirani ya Afrika mashariki na kati, pamoja na kuwakera wafadhili.

Katibu mkuu wa zamani wa umoja wa mataifa Kofi Annan anatarajiwa kwenda Kenya kesho Jumanne akiongoza kundi la viongozi wenye busara kutoka mataifa ya Afrika ili kujaribu kuazisha majadiliano baina ya Kibaki na kiongozi wa upinzani Raila Odinga , ambao hawajakutana tangu kumalizika kwa uchaguzi.