1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Annan na juhudi za amani nchini Kenya

Mwakideu, Alex15 Februari 2008

Vyama vinavyozoza nchini kenya vimekubaliana kuibatilisha Katiba ya nchin hiyo ili upinzani ushirikishwe katika serikali.

https://p.dw.com/p/D856
Mpatanishi Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa mataifa Kofi Annan.Picha: AP


Hatua hiyo imetajwa kuwa kubwa katika juhudi za kumaliza ghasia zilizosababisha vifo vya zaidi ya watu elfu moja katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.


Katibu mkuu wa zamani katika Umoja wa Mataifa Koffi Annan anatarajiwa kutangaza leo maelezo kamili kuhusu makubaliano hayo yaliyotiwa sahihi wajumbe wanaomwakilisha Rais Mwai Kibaki na kiongozi wa upinzani Raila Odinga anaedai kwamba uchaguzi wa mwezi disemba ulikumbwa na udanganyifu.


Mazungumzo ya upatanisho yanayoongozwa na Annan yanatarajiwa kuendelea jumatatu atakapowasili waziri wa nchi za nje wa Marekani Condoleeza Rice na ujumbe wake kwa viongozi wa Kenya kwamba lazima demokrasia irejee nchini humo.


Kichwa katika gazeti la Daily Nation nchini Kenya hii leo kilikuwa ni "Ujumbe unaoongozwa na Annan wakamilisha nusu ya mazungumzo ya upatanisho" nalo gazeti la The Standard lilikuwa na kichwa "saa arobaini na nane baadaye na makubaliano bado hayajapatikana"


Ghasia nchini Kenya zilianzia pale Kibaki mwenye miaka sabini na sita alipotangazwa mshindi wa uchaguzi wa disemba tarehe ishirini na sabaambao upinzani unadai ulikumbwa na utata.


Waangalizi wa kimataifa nao wanasema kulikuwa na udanganyifu katika shughuli ya kuhesabiwa kwa kura.


Kulingana na shirika la msalaba mwekundu nchini Kenya zaidi ya watu elfu moja wameuwawa katika maandamano, vita vya kikabila na makabiliano ya polisi na watu wengine laki tatu wameachwa bila makao; jambo ambalo limeharibu sifa za nchi hiyo iliyokuwa ikijulikana kama moja wapo wa nchi tulivu na zenye demokrasia.


Annan amekuwa akisisitiza ugavi wa mamlaka kati ya serikali na upinzani ambao utauleta pamoja upinzani na serikali na kuzipatia pande hizo mbili wakati wa kutayarisha uchaguzi mwengine baada ya miaka miwili.


Lakini upande wa serikali umekuwa ukipinga mpango wa kugawa mamlaka na upinzani huku ukisema kwamba unaweza kuwaingiza viongozi wa upinzani serikalini ikiwa watakubali kuwa chini ya mamlaka ya Rais Mwai Kibaki.


Upinzani nao umekuwa ukisisitiza kwamba Raila Odinga anapaswa kupewa mamlaka ya waziri mkuu mwenya atakaekuwa kiongozi wa serikali; nafasi ambayo italazimu kubatilishwa kwa katiba ya Kenya.


Hata hivyo pande hizo mbili zimekubaliana kuanzisha shughuli ya marekebisho ya katiba itakayochukua mwaka mmoja na ambayo inanuiwa kumaliza tofauti zilizosababisha ghasia nchini humo.


Nimezungumza na Daktari Ekuru ambaye ni wakili na mhadhiri katika chuo cha uwakili mjini Nairobi kuhusu kubadilishwa kwa katiba na iwapo swala hilo litakubaliwa na wakenya hata katika siku za usoni.

Lakini afisa mmoja anaeshiriki katika mazungumzo ya upatanisho na ambaye hakutaka kutajwa jina lake amesema shughuli hiyo ya marekebisho ya katiba haitaanza hadi watakapokubaliana kuunda serikali inayoshirikisha upinzani. Wajumbe wameonekana kushindwa kukubaliana kuhusu serikali ya aina hiyo.


Waziri wa sheria na maswala ya katiba Martha Karua ambaye pia anawakilisha serikali katika mazungumzo ya upatanisho amesema makubaliano mwafaka hayajafikiwa lakini mazungumzo yanaendelea.


Hata hivyo mkataba wa makubaliano uliotiwa sahihi na pande wawakilishi wa serikali na upinzani katika mazungumzo hayo unatarajiwa kuwekwa wazi leo.


Kibaki amekuwa akishinikizwa na jamii ya kimataifa kurejesha utulivu na demokrasia nchini Kenya huku Marekani na Uingereza zikitishia kuwawekea vikwazo vya usafiri viongozi waliosababisha ghasia nchini Kenya.


Rais wa Marekani George Bush alisikika akisema kwamba amemtuma waziri wa nchi za nje Condoleeza Rice nchini Kenya aende kuunga mkono juhudi za upatanishi zinazoongozwa na Annan.


Rice anatarajiwa kuzungumza na Kibaki pamoja na Odinga na pia kukutana na viongozi wa mashirika ya kijamii na wafanyibiashara mjini Nairobi siku ya jumatatu.


Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Koffi Annan amekuwa akiendeleza mazungumzo ya upatanishi katika hoteli moja kusini mwa Kenya kunzia jumanne wiki hii katika harakati za kutafuta maelewano kando na vyombo vya habari.