1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ARUSHA : Waasi wa Dafur wataka mazungumzo na serikali

6 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBbf

Makundi ya waasi wa Dafur yanayokutana katika mji wa Arusha Tanzania yanataka mazungumzo ya mwisho ya amani na serikali ya Sudan yafanyike katika kipindi cha miezi michache ijayo.

Jan Eliasson mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa suala la Dafur amesema kwamba waasi hao wamependekeza kwamba mazungumzo hayo ya mwisho yanapaswa kufanyika kati ya miezi miwili hadi mitatu kuanzia sasa.

Waasi hao wa Dafur leo wanakamilisha mazungumzo yao yenye lengo la kuwa na msimamo wa pamoja kabla ya kuanza mazungumzo na serikali ya Sudan na hiyo kuimarisha zaidi matumaini ya amani ikiwa ni wiki moja kufuatia uamuzi wa Umoja wa Mataifa kupeleka kikosi kikubwa cha kulinda amani Dafur.

Mazungumzo hayo ya mwishoni mwa juma chini ya usuluhishi wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika awali yalikuwa yamepangwa kumalizika hapo jana.