1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ARUSHA:Mazungumzo ya kusaka amani ya Darfur yaendelea nchini Tanzania

4 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBc9

Viongozi wa makundi ya waasi nchini Sudan wako katika wanaendelea na mazungumzo yao ya kutafuta suluhu la mzozo wa Darfur.

Mazungumzo hayo yanayofanyika mjini Arusha nchini Tanzania yako chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika mzozo huo Jan Eliasson alielezea matumaini yake ya kufikiwa kwa muafaka na serikali ya Sudan mnamo mwisho wa mazungumzo hayo.

Hata hivyo kundi kubwa la waasi limesusia mazungumzo hayo likidai mambo kadhaa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alikiita kipindi kijacho kuwa ni muhimu katika majaaliwa ya Dafur.

Katika taarifa yake kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu huyo alitahadharisha kuwa kuendelea kwa hali ya uhasama kwenye eneo hilo, juhudi za kutafuta suluhu la kisiasa na kupatikana kwa amani hazitafanikiwa.

Takriban watu laki mbili inaaminika wameuawa na wengine zaidi ya milioni mbili hawana makazi toka mzozo huo wa Darfur ulipoibuka miaka minne iliyopita.