1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ASEAN kuepuka ugomvi kuhusu bahari ya Kusini mwa China

John Juma
13 Novemba 2017

Viongozi kutoka nchi 10 wanachama wa Jumuiya ya mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia ASEAN pamoja na China walijadili mkataba unaohusu shughuli zao

https://p.dw.com/p/2nXuZ
Vietnam chinesicher Präsident Xi Jinping in Hanoi
Picha: picture-alliance/AP Photo/Hoang Dinh Nam

Vietnam na China zimekubaliana kuepuka ugomvi katika eneo linalozozaniwa la bahari ya Kusini mwa China kama njia mpya ya kuwezesha mazungumzo ya viongozi wa nchi zaeneo hilo  ili kupunguza hali ya  wasiwasi.

Nchi hizo mbili jirani na za kikoministi zimekuwa katika mvutano kuhusu bahari ambayo huwezesha biashara ya dola trilioni tano kila mwaka na ambayo inaaminika kuwa na utajiri mkubwa wa gesi.

Katika taarifa ya pamoja, baada ya rais wa China Xi Jinping kuitembelea Vietnam , Vietnam na China zimekubaliana kudumisha Amani katika bahari hiyo.

Mkataba wa kumaliza ugomvi

Katika mkutano uliofanyika mji mkuu wa Ufilipino-Manila na kufunguliwa na rais wa nchi hiyo Rodrigo Duterte, viongozi kutoka nchi 10 wanachama wa Jumuiya ya mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia ASEAN pamoja na China walijadili mkataba unaohusu shughuli zao, ambapo walielezea matumaini kuhusu mustakabali wa mahusiano yao.

Wamekubaliana kusimamia vyema mizozo ya bahari, kutochukua hatua zinazoweza kutatua au mizozo na pia kudumisha Amani katika Bahari ya Mashariki.

Rais Trump ashangaa alipogundua anasalimiana tofauti na jinsi viongozi wa ASEAN husalimiana
Rais Trump ashangaa alipogundua anasalimiana tofauti na jinsi viongozi wa ASEAN husalimianaPicha: picture-alliance/dpa/A. Harnik

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa kutoka upande wa Vietnam kuhusu maafikiano hayo. Viongozi hao pia watasaini mkataba wa kulinda wafanyakazi wahamiaji wanaotoka nchi maskini katika kanda hiyo.

China yadai umiliki wa bahari hiyo

China inadai takriban bahari hiyo yote na hata kukaribia fukwe za nchi jirani. Katika miaka ya hivi karibuni China imeunda kisiwa na kujenga uwanja mdogo wa wa ndege unaoweza kutumiwa kijeshi katika eneo hilo linalozozaniwa ili kuimarisha udhibiti wake, hali ambayo imezusha wasiwasi  miongoni mwa mataifa jirani.

Kumekuwa na mizozano ya kivita mara mbili kati ya China na Vietnam baharini mnamo 1974 na 1988 ambapo wanajeshi kadhaa wa Vietnam waliuawa.

Trump ashiriki mikutano na viongozi wa ASEAN

Mapema wiki hii, rais wa Marekani Donald Trump alikuwa mjini Manila kwa mikutano na viongozi wa ASEAN na nchi nyingine ambapo pia ndicho kituo chake cha mwisho katika ziara yake barani Asia.

Katika wa Jumuiya ya ASEAN, China na Jumuiya hiyo ambamo Vietnam pia ni mwanachama zilitangaza kuwa zimekubaliana kuanzisha mazungumzo kuhusu mkataba wa shughuli zao katika bahari hiyo ya Kusini mwa china.

Kwa mujibu wa kituo cha televisheni kinachomilikiwa na serikali ya China Waziri Mkuu wa China Li Keqiang aliridhia mkataba wa viongozi wa ASEAN. Hata hivyo hakuna muda maalum ambao ulitolewa kuhusu kuwepo kwa mkataba kamili.

Mwandishi: John Juma/AFPE/DPAE

Mhariri: Mohammed Abdul-rahman