1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Asilimia 21 ya spishi za mimea hatarini kutoweka

Iddi10 Mei 2016

Ripoti ya kwanza ya kina inayoangazia maisha ya mimea ya dunia imeeleza kuwa moja kati ya aina tano za mimea uko hatarini kutoweka kutokana kubadilishwa kwa matumizi ya ardhi.

https://p.dw.com/p/1IlGk
Bildergalerie Fleischfressende Pflanzen
Picha: Getty Images

Utafiti uliyopewa jina la "Hali ya mimea ya dunia" umesanifiwa kutoa msingi wa ulinganifu kwa ripoti za kila mwaka zitakazokadiria ni spishi ngapi za mimea zinagunduliwa na ni ngapi zinapotea milele.

Kwa ujumla aina 391,000 za mimea zinajulikana kwa wanasayansi, kuanzia mimea midogo ya maua hadi miti mikubwa kabisaa, kulingana na ripoti hiyo ilioandaliwa na wataalamu 80 wakiongozwa na Bustani ya mimea ya Royal RBG, iliyoko Kew mjini London.

Na licha ya ukweli kwamba asilimia 21 ya spishi hizi zinakabiliwa na kitisho cha kutoweka, ripoti hiyo ilisema mimea mipya inaendelea kugunduliwa, kwa mfano mmea wenye urefu wa mita 1.5 unaokula wadudu uliogundulika kwenye kilele cha mlima nchini Brazil mwaka 2015.

Pamoja na hayo, wataalamu wamesema sehemu nyingi za dunia zinapitia mabadiliko makubwa, kama vile kukatwa kwa misitu kupisha kilimo na ujenzi wa miji. Joto dunia lilitajwa kuwa miongoni mwa hatari zinazosababishwa na shughuli za kibinaadamu.

Wanandoa wakihudumia mimea yao nchini Ujerumani.
Wanandoa wakihudumia mimea yao nchini Ujerumani.Picha: Rido - Fotolia.com

"Zaidi ya asilimia 10 ya ardhi ya dunia imebadilishwa matumizi katika kipindi cha miaka 10 iliyopita. Kuna mabadiliko makubwa yanaendelea, hasa mabadiliko ya kilimo na ardhi kwa ajili ya ujenzi wa miji," alisema Profesa Kathy Willis, mkurugenzi wa Bustan ya Royal RBG iliyoko Kew mjini London.

Mimea kwa matumizi anuwai

Alisema kinachohitajika ni kuwa na mawazo yakinifu: "Namaanisha kuwa tuna idadi ya watu iliyoongezeka, wanahitaji chakula, wanahitaji mahala pa kuishi, hivyo jambo halisi tunalohitaji kufanya ni kuainisha ni maeneo yepi muhimu ya kihafadhi kwa sababu ya aina mbalimbali za mimea yaliyonazo, na maeneo yepi tunapaswa kuendeleza."

Ripoti hiyo ilisema spishi za mimea 31,000 zina matumizi yalioainishwa kama vile ya kitabibu, chakula au vifaa vya ujenzi. Mimea isiyojulikana sana, inaweza kuwa faida kama vile kuhimili magonjwa. Professa Willis alisema jambo zuri ni kwamba wanagundua mimea mingi mipya - karibu 2,000 kila mwaka, ikiwemo ya chakula, kwa ajili ya mafuta au dawa.

Lakini kwa upande mwingne, mkurugenzi huyo wa sayansi wa RGB, kuwa kumekuwa na mabadiliko makubwa katika matumizi ya ardhi yakisukumwa hasa na shughuli za kitamaduni, zikichagizwa kwa sehemu ndogo na mabadiliko ya tabianchi. Alisema lengo ni kupata uelewa zaidi wa mambo yanayopelekea mabadiliko hasi, na kuyabadili ili kulinda mimea zaidi dhidi ya kutoweka.

"Tuna mahitaji makubwa ya chakula hivyo kuna midomo mingi sana ya kulisha duniani kwa sasa na idadi hiyo inaongezeka na tunahitaji ardhi, hivyo makaazi asili yanabadilishwa ili tuwe na mashamba ya soya, mazao, mifugo na matokeo yake ni kwa spishi kupoteza makaazi yake na kusogea karibu na kutoweka," alisema Mtafiti wa uhifadhi kutoka RGB Steve Bachman.

Mmoja wa mimea inayotumiwa kwa ajili ya dawa.
Mmoja wa mimea inayotumiwa kwa ajili ya dawa.Picha: Fotolia/steheap

Mkakati imara wahitajika

Hivyo anasema kuwa na mkakati mpana na mnyumbulifu zaidi kwa uzalishaji wa mazao yetu kunamaanisha kujiimarisha kwa ajili ya changamoto za wakati ujao, hasa mabadiliko ya tabianchi, magonjwa zaidi, wadudu zaidi wanaoiambukiza mimea, ambayo yote yana uwezekano mkubwa wa kutokea.

Karibu aina 2,000 za mimea mipya zinaedelea kutolewa maelezo kila mwaka. Mmea unaopatikana katika eneo la Minas Gerais nchini Brazil, unaojulikana kama drosera magnifica, ni mmoja ya mimea mikubwa zaidi inayojulikana kwa kula wanyama. Uligunduliwa na mtaalamu wa mimea ya drosera, wakati akichunguza picha kwenye mtandao wa facebook zilizochukuliwa na muwindaji wa okadi.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre, ape

Mhariri: Mohammed Khelef