1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Askofu wa zamani ashinda uchaguzi mkuu Paraguay

Kalyango Siraj21 Aprili 2008

Avunja ukiritimba wa chama wa zaidi ya miongo 6 madarakani

https://p.dw.com/p/DlYz
Askofu wa zamani wa kikatoliki Fernando Lugo, katikati kulia , akiwa na mgombea mwenza Federico Franco, katikati kushoto wakiinua mikono yao juu wakisalimu wafuasi mjini Asuncion, jumpili, April 20, 2008. Lugo ameshinda uchaguzi wa historia ambao umemaliza miaka 60 ya chama kimoja The Colorado Party.Picha: AP

Askofu wa zamani avunja daftari ya historia katika nchi ya Paraguay kwa kushinda uchaguzi wa rais.Fernando Lugo amepata asili mia 41 ya kura zilizohesabiwa na hivyo kumshinda mtetezi wa chama kilichokuwa madarakani kwa asili mia 10.Upande wa serikali umekubali kuwa umeshindwa.

Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 60 na Ushei nchi ya Paraguay imepata kiongozi kutoka upande wa upinzani.

Paraguay ni taifa linalopatikana katika bara la Amerika Kusini. Miongni mwa mataifa maarufu linalopakana nalo ni Brazil,upande wa kaskazini na Argentina upande wa kusini.

Taifa la Paraguay limekuwa likitawaliwa na chama kimoja mfululizo cha The Colorado Party tangu mwaka wa 1947.

Sasa ukiritimba huo umevunjwa.

Na ushindi wa mwishoni mwa juma wa Askofu wa walala hoi,kama anavyojulikana wakati mwingine,ndio umeleta kikomo cha utawala mrefu kuwahi kutokea wa chama kimoja duniani hususan cha wahafidhina.

Kiongozi mpya wa Paraguay,Fernando Lugo, anajulikana kama mtu anaetetea maslahi ya walala hoi na ni mtu wa siasa za mrengo wa kati -kushoto. Anaongoza mseto wa vyama unaounganishwa katika chama kimoja cha Patriotic Alliance for Change.

Baada ya kutangazwa na tume kama mshindi aliwahutubia wafuasi wake walikuwa katika makao makuu ya chama chake mjini Ansocion akisema kuwa sasa imedhirisha kuwa hata watu wachahce wanaweza kushinda.

Tume ya uchaguzi imemtangaza kama mshindi aliepata asili mia 41 ya kura ikilinganishwa na mpinzani wake Bi Blanca Ovelar wa chama tawala cha Colorado Party kilichopata asili mia 31.

Ikiwa chama tawala kingeshinda mgombea wake ndie angekuwa mwanamke wa kwanza kuwa rais katika bara la Amerika ya Kusini.

Lakini ndoto zake hizo hazikutimia,na badala yake nyota ya Askofu wa walala hoi ndio imepanda.

Mshindi Hugo, alizaliwa mwaka wa 1951,na kuanza upadri mwaka wa 1977.Alifanya kazi ya kimisheni kwa miaka mitano katika nchi ya Ecuador.Mwaka wa 1994 alitawazwa kama Askofu na kufanya kazi hiyo kwa kipindi cha miaka 10 katika eneo la watu maskini la San Pedro,na huko ndiko alikopewa jina la kupanga la Askofu wa walala Hoi kwa kuwa ndiko alipigania maslahi ya watu ambao hawakuwa na ardhi.

Umaarufu wake kitaifa ulikuja Machi mwaka wa 2006 aliposaidia kuongoza mkutano mkubwa wa upande wa upinzani katika mji mkuu wa nchi hiyo wa Ansuncion.

Disemba mwaka huo alijiuzulu kama Padri,lakini Vatican ilikataa kujiuzulu kwake ikisema kuwa kazi ya Upadri ni ya maisha na badala yake kanisa katoliki ilimsimamisha kwa mda.

Katiba ya Paraguay inawapiga marufu mtu anaejihusisha katika masuala ya kidini kuingia katika masuala ya kisiasa.

Hugo anapenda kujiiita kama mtu wa kati japo anaunga mkono mageuzi kuhusu umilikaji wa ardhi na pia njia zingine za kupigana dhdi ya umaskani.

Hata hivyo amejitenga na viongozi wa mrengo wa kushoto maarufu kama vile rais Hugo Chavez wa Venezuela na rais Evo Morales wa Bolivia.

Ingawa anasema kuwa hajihisi kama mtu wa mrengo wa kushoto lakini anawakilisha changamoto kubwa ya nchi hiyo ya kutokuwa na usawa wa kijamii.

Azma yake kuu ni kujadilia upya mikakati ya miradi miwili ya mabwawa mawili ya kuzalisha umeme.Sana sana anataka Brazil kulipa pesa zaidi za umeme inayotumia kutoka katika bwawa la umeme la Itaipu wanalomiki kwa ubia .Bwawa hilo ndilo kubwa zaidi duniani.

Lugo anasema kuwa ataishtaki brazil katika mahakama ya kimataifa mambo yakishindikana.

Rais wa sasa Nicanor Duarte ambae katiba inazuia kugombea muhula meingine amesema yuko tayari kumsaidia bw Lugo na kusema kuwa uchaguzi huo pia umevunja daftari nyingine ya kuwa kwa mara ya kwanza nchi hiyo chama kimoja kitakabidhi madaraka kwa chama kingine bila mapinduzi ya kijeshi wala umwagaji damu.