1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Assad awasifu wanajeshi wake

1 Agosti 2012

Rais Bashar al-Assad wa Syria amesema kwamba vita kati ya jeshi la nchi yake na waasi vitaamua hatima ya Syria. Amewapongeza pia wanajeshi wake kwa kupambana na kile alichokiita makundi ya magaidi wahalifu.

https://p.dw.com/p/15hac
Wanajeshi wa Syria
Wanajeshi wa SyriaPicha: Reuters

Katika tamko alilolitoa kwenye maadhimisho ya siku ya jeshi nchini Syria, rais Assad alisema kwamba hatima ya raia wa nchi hiyo, pamoja na taifa, kwa ujumla, inategemea vita vinavyoendelea kati ya waasi na wanajeshi wa Syria. Tangu kuuwawa kwa maafisa wakuu wa nne wa jeshi lake wiki mbili zilizopita, Assad hajazungumza tena hadharani. Assad aliwasifu wanajeshi wake na kusema kwamba ana imani kubwa na kile wanachokifanya.

Mapigano kati ya jeshi la Syria na waasi sasa yanaripotiwa kufika katika makaazi ya wakristo kwenye mji mkuu wa Damascus. Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu nchini Syria, lenye makao yake makuu London, Uingereza, mapigano yamezuka leo asubuhi katika baadhi ya viunga vya Damascus ambapo kwa miaka mingi wamekuwa wakiishi waumini wa dini ya Kikristo. Mkuu wa shirika hilo, Rami Abdelrahman, amesema hii ni mara ya kwanza kwa machafuko kufika katika maeneo hayo. Zipo ripoti kwamba tayari askari mmoja ameshauwawa huko.

Wakaazi wa Aleppo wakimbilia misikitini na mashuleni

Katika mji wa Aleppo, ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini Syria, miripuko ya mabomu, milio ya risasi na makombora ilisikika usiku wa kuamkia leo. Waasi wamesema kwamba walifanikiwa kuwafukuza wapiganaji wa jeshi la Assad kutoka katika baadhi ya maeneo. Kamanda mmoja wa waasi amesema lengo lao ni kuingia katikati ya mji wa Aleppo na wanataka kufanya hivyo kwa kuteka kitongoji kimoja baada ya kingine cha mji huo. Wakati mapigano yakiendelea, idadi ya wakimbizi nayo inapanda siku hadi siku.

Wakaazi wa Aleppo wakiukimbia mji wao
Wakaazi wa Aleppo wakiukimbia mji waoPicha: Reuters

Wakaazi wa Aleppo wanaoshindwa kuukimbia mji wao wanatafuta hifadhi katika misikiti, mashuleni na kwenye majengo ya vyuo vikuu. Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, Melissa Fleming, amesema kuwa watu hawa wanategemea misaada. "Tunajaribu kila liwezekanalo kuwapatia misaada watu waliokimbilia mashuleni. Kulingana na taarifa tulizopokea, watu kati ya 250 na 350 wamepatiwa hifadhi katika kila shule ya mjini Aleppo," alisema Flemming. "Kwenye mabweni ya vyuo vikuu wapo watu wengine wapatao 7,000 waliokimbia vita na machafuko katika mitaa ya Aleppo."

Wakati huo huo, mkuu wa jeshi huru la Syria amelaani hatua ya kuundwa kwa kundi jipya la kisiasa nje ya Syria, lenye lengo la kuanzisha serikali ya mpito. Kundi hilo linalojiita baraza la mapinduzi la Syria liliundwa jana huko Cairo, Misri, na wanaharakati 70 kutoka Syria wanaoishi uhamishoni.

Mwandishi: Elizabeth Shoo

Mhariri: Othman Miraji