Assad kuhutubia taifa leo
20 Juni 2011Hotuba hii inakuja baada ya wanaharakati wa upinzani kutangaza kuwa wanaunda baraza la taifa, ili kuratibu mapambano dhidi ya utawala wa Rais Assad.
Itakuwa ni mara ya tatu kwa Assad kutoa hotuba muhimu tangu maandamano yanayodai uhuru zaidi pamoja na demokrasia kuzuka nchini Syria katikati ya mwezi Machi 2011.
Jana Jumapili, majeshi ya Syria yaliingia katika eneo la mpaka wa kaskazini magharibi kuwazuwia raia wa nchi hiyo wanaokimbilia nchini Uturuki. Wanaharakati wa haki za binadamu wamesema kuwa maelfu ya raia ambao wamekuwa wakikimbia wamekwama na wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada waliokuwa wakijaribu kuwapa chakula na mahitaji mengine wameshambuliwa na majeshi ya serikali.
Shambulio la hivi karibuni kabisa linafuatia maandamano makubwa nchini Syria siku ya Ijumaa, wakati wanaharakati wa haki za binadamu wanasema majeshi ya usalama yamewauwa waandamanaji zaidi ya 19.