1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Assad kutumia silaha za sumu dhidi ya waasi?

5 Desemba 2012

Waasi wameizingira kambi moja ya kikosi cha anga karibu na Damascus, wakati Marekani ikieelezea wasi wasi wake kwamba Rais Bashar al Assad wa Syria anayetapatapa huenda akatumia silaha za sumu kukabiliana na upinzani.

https://p.dw.com/p/16wKr
Mzozo wa Syria
Mzozo wa SyriaPicha: Reuters

Clinton amesema leo hii kwamba Marekani ina wasi wasi kuwa Rais Bashar al Assad wa Syria ambaye anazidi kutapatapa anaweza kuamuwa kutumia silaha za sumu au kupoteza udhibiti wake kwa silaha hizo.Baada ya kukutana na mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya NATO mjini Brussels Ubelgiji ambapo jumuiya hiyo ya kijeshi ya mataifa ya magharibi imekubali kupeleka Uturuki nchi jirani na Syria makombora ya kujihami ya patriot ambapo hutumika kudukiza makombora yanayorushwa kutoka nje, Clinton amesema serikali ya Marekani imeweka wazi kwa Syria kwamba Marekani itabidi kuchukuwa hatua iwapo nchi hiyo itatumia silaha za sumu.

Clinton ameuambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Brussels kwamba wasi wasi wao Assad anayezidi kutapa huenda akaamuwa kutumia silaha za sumu au akapoteza udhibiti wa silaha hizo kwa mojawapo ya makundi mengi ambayo hivi sasa yanaendesha harakati zake nchini humo.Waasi nchini Syria wamesema leo hii kwamba wameizingira kambi moja ya kikosi cha anga karibu na mji mkuu wa Damascus ikiwa ni ishara mpya kwamba mapigano hayo hayo yanazidi kuunyemelea mji mkuu huo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton.Picha: dapd

Mapigano yapamba moto

Mapigano makali yamezuka karibu na mji wa Damascus wiki moja iliopita na kuvikisha vita hivvyo kwenye kitovu cha utawala wa Assad ambapo huko nyuma vilikuwa vikipiganwa kwenye majimbo. Wapiganaji wamesema wameizunguka kambi ya kikosi cha anga ya Aqraba ilioko kama kilomita 4 nje ya mji mkuu.Abu Nidal msemaji wa kikosi cha wapiganaji waasi cha Habib al Mustafa amesema wanataraji kuiteka kambi hiyo masaa machache yajayo.Ameongeza kusema kwamba waasi wamekiteka kituo cha wanajeshi wa anga kilioko karibu na hapo na kimeuwa wanajeshi kadhaa,kuwatia nguvuni wengine na wengine kadhaa wameweza kukimbia.Habari kama hizo kutoka Syria imekuwa vigumu kuzithibitisha kutokana na serikali kuzuwiya vyombo vya habari kurepoti nchini humo.

Mkakati wa wanajeshi ni kuigawa Damascus makao makuu ya utawala wa Assad kutoka viunga vilioko nje ya mji huo ambapo waasi wamekuwa wakizidi kuvidhibiti. Mashambulizi ya anga yamekuwa yakiendelea kwa zaidi ya wiki moja dhidi ya viunga hivyo ambapo wanaharakati wanasema ni mashambulizi makubwa kuwahi kushuhudiwa kwenye viunga hivyo.

Mojawapo ya viunga vya Damascus vilivyoshambuliwa na ndege za Assad.
Mojawapo ya viunga vya Damascus vilivyoshambuliwa na ndege za Assad.Picha: Reuters

Duru za serikali ya Syria zimesema jeshi limeweza kuwarudisha nyuma waasi kwa kilomita 9 kutoka mji mkuu. Waasi hawakuthibitisha wala kukanusha habari hizo lakini wamesema lengo lao haliko katika kuingia wenye mji huo kwa sasa.

Makobombora ya Kujihami kwa Uturuki

Kwa upande mwengine uamuzi wa NATO wa kutuma makombora ya kujihami ya Marekani, Ujerumani na Uholanzi kusaidia kuulinda mpaka wa Uturuki utavifikisha vikosi vya Marekani na Ulaya kwenye mpaka wa Uturuki kwa mara ya kwanza kabisa katika mzozo huo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria viliodumu kwa miezi 20 sasa.

Aina ya makombora ya "Patriot " yatakayowekwa katika mpaka wa Uturuki na Syaria.
Aina ya makombora ya "Patriot " yatakayowekwa katika mpaka wa Uturuki na Syaria.Picha: dapd

NATO imesema makombora hayo inayoyatuma Uturuki ni kwa ajili tu ya kujihami lakini Syria na washirika wake wa Urusi na Iran wameushutumu uamuzi huo kwa kusema kwamba unazidisha hali ya ukosefu wa utulivu katika eneo hilo.

Mwandishi: Mohammed Dahman/AFP/Reuters

Mhariri: Mohamed Khelef