1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Athari badala ya faida

Maja Dreyer11 Oktoba 2006

Tangu mazungumzo ya Shirika la Biashara Duniani WTO kuhusu nchi zinazoendelea kusimamishwa, Umoja wa Ulaya unaendesha mazungumzo na nchi zilizokuwa makoloni ya baadhi ya mataifa wanachama wa umoja huo barani Afrika na kutoka maeneo ya Caribian na Pacific, kwa ufupi nchi za ACP.

https://p.dw.com/p/CHmP
Chai ya maziwa ya kienyeji au ya unga ya maziwa kutoka Ulaya?
Chai ya maziwa ya kienyeji au ya unga ya maziwa kutoka Ulaya?Picha: Freefoto

Kinachopendekezwa ni maafikiano mapya ya biashara huru kati ya Ulaya kwa jumla na nchi moja moja za ACP. Wakosoaji lakini wanasema maafikiano kama haya yanaweza kuathiri masoko ya nchi maskini.

Tangu mwaka wa 1973 nchi za Ulaya zimetoa msaada wa maendeleo na haki fulani ya biashara huru kwa nchi zinazoendelea za kundi la ACP. Haya yalikuwa ni maafikiano yaliyojulikana kama mikataba ya Lomé na Cotonou. Mikataba hiyo ilizinufaisha nchi za ACP, lakini haikufuata sheria za shirika la biashara duniani, WTO. Kwa sababu hiyo, Umoja wa Ulaya na nchi za ACP zinatakiwa kutafuta makubaliano mapya. Kulingana na maafikiano ya ushirikano wa kiuchumi, kwa ufupi, EPA, kama yaliyopendekezwa na Umoja wa Ulaya, pande zote mbili zinatakiwa kufungua mipaka yao kwa biashara huru pamoja na kupunguza ushuru wa forodha.

Kwa maoni ya Douglas Kivumbi lakini, makubaliano haya mapya ya EPA yataziathiri vibaya nchi za Kiafrika. Bw. Kivumbi ni mtaalamu wa mambo ya kiuchumi wa taasisi ya uchumi na biashara SEATINI yenye makao yake makuu nchini Uganda. Naye anasema ikiwa vyakula vya kutoka Ulaya vilivyotengenezwa kwa kiwango cha juu vitauzwa katika nchi za Afrika, basi viwanda na wakulima wa kienyeji vitashindwa kabisa.

Mfano ni nchi ya Uganda ambapo wateja wanaweza kupata unga ya maziwa ya bei ya chini kuliko kununua maziwa ya kawaida. Amesema: “Ikiwa bidhaa kama hizo zitaweza kuingia katika soko huru kama inavyopendekezwa katika makubaliano haya ya EPA, sekta yetu ya ufugaji itaharibika, kwani bidhaa hizo ni rahisi kuliko maziwa ya kienyeji. Hakuna hata mkulima mmoja ambaye ataweza kushindana katika soko huru.”

Juu ya hayo kupunguzwa kwa ushuru wa forodha kutaziathiri bajeti za nchi zinazoendelea kwani zinategemea mapato ya forodha kwa kiwango kikubwa. Vile vile muda wa kufungua soko ambao unatakiwa kufanyika baada ya miaka kumi, unakosolewa kuwa ni mfupi mno.

Kwa sababu hizo mashirika kadhaa yanadai, maslahi ya nchi maskini yapewe umuhimu zaidi katika makubaliano haya. Hata nchi kama Afrika Kusini ambayo ina nguvu mkubwa za kiuchumi, haina vifaa vya kutosha vya kuzishurutisha nchi za Ulaya na kuimarisha maslahi yake, anasema Malcom Duncan wa shirika la usawa wa kiuchumi la Afrika Kusini. Alitoa mfano wa ushuru mkubwa wa forodha kwa bidhaa zilizotengenezwa katika viwanda vya Kiafrika.

Bw. Duncan anaeleza: “Nchi za Ulaya zinataka mali ghafi. Hazitaki kwamba nchi za Afrika ziweke thamani zaidi katika bidhaa zake kwa kutumia mali ghafi katika viwanda. Ukifanya hivyo, basi ushuru wa forodha utapanda juu. Badala yake nchi za Ulaya zenyewe zinatumia mali hizo na kutengeza bidhaa za bei ya juu na kuziuza tena katika nchi za Kiafrika. Hii si sawa.”

Pamoja na soko la kiuchumi, nchi za Ulaya zinataka pia soko la huduma za kijamii lifunguliwe – jambo ambalo limeshakataliwa na nchi zinazoendelea katika mazungumzo ya WTO. Licha ya mivutano hiyo yote, Umoja wa Ulaya unataka mazungumzo kuhusu makubaliano ya EPA yamalizike hadi ifikapo mwishoni wa mwaka huu.