1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Athari za mgogoro wa kiuchumi

Charo Josephat 16 Februari 2009

Je nchi zinaweza kuwa muflisi kutokana na kuporomoka kwa uchumi?

https://p.dw.com/p/GvT5

Matatizo ya kifedha yanayozikabili benki yanaendelea na tayari ni hali ambayo inakaribia kuzoeleka. Imewashangaza wengi kwamba mgogoro huu wa kiuchumi unaoikabili dunia unaweza kuifanya nchi nzima kuwa muflisi. Iceland ni nchi ndogo yenye wakaazi 300,000 tu. Haijafikia kiwango cha kufilisika, lakini bila misaada kutoka nje, mambo hayaendi tena sawa katika kisiwa hicho.

Nchi nyingi duniani zinakabiliwa na madeni makubwa huku zikiwa bila matumaini ya kuweza kulipa. Hata hivyo kwa kawaida inasemekana kuwa nchi haziwezi kwenda muflisi kwa sababu ya uwezo wake mkubwa ilionao ikilinganishwa na kampuni. Hiyo si sahihi anasema Christopher Ohler, profesa wa sheria na maswala ya uchumi katika chuo kikuu cha Jena.

"Kihistoria mara kwa mara nchi zimewahi kuwa muflisi. Katika nyakati za hivi karibuni kwa mfano Ukraine au Argentina zimetumbukia katika hali ya kutoweza kulipa madeni. Tofauti muhimu kati ya kufilisika binafsi ni kufilisika kwa nchi, ni kwamba nchi haziwi mara kwa mara muflisi. Mara nyingi nchi huwa katika hali ya kutoweza kulipa madeni hivyo kushindwa kutimiza majukumu yake. Bila kuzingatia muda wa nchi kupata ahueni ya kiuchumi, baada ya miaka kadhaa malipo huanza kulipwa tena na nchi kujiimarisha tena katika masoko ya fedha ya kimataifa."

Ikiwa nchi inafanya vizuri, au vibaya au iko katikati katika ulipaji wa madeni, ni tathimini inayofanywa na mashirika ya Standard & Poor na Moody´s. Mashirika haya hulinganisha mapato na matumizi ya nchi, sawa na kampuni, anasema Alexander Kockberck, mchanganuzi wa shirika la Moody´s mjini Frankfurt hapa Ujerumani.

"Kwa kweli ndio maana hali ni tofauti kwa sababu serikali ina uwezo wa kubadili mikataba. Inaweza kwa mfano kubadili sheria kuhusu kodi, bila shaka kupitia msaada wa bunge. Nchi ina upeo mkubwa wa kuchagua jinsi ya kulinda mapato yake kuliko kampuni."

Kwa muda mrefu nchi ya Iceland imekuwa mfano wa nchi yenye madeni makubwa na ilipewa maksi mazuri na shirika la Moody´s kwa kupata AAA. Christoph Ohler, mwanasheria wa maswala ya kiuchumi anasema Iceland ni nchi yenye wakaazi 300,000 na uchumi wake ni mdogo. Mbali na uvuvi uchumi huo unategemea benki tatu za kimataifa ambazo katika miaka iliyopita, zimepanuliwa mno. Madeni yanayozikabili benki hizi hayawezi kulipwa tena kwa kuwa katika masoko ya fedha ya kimataifa benki hizo hazistahili kupata mikopo.

Serikali ilitangaza kuzitaifisha benki hizo tatu ikisema iko tayari kubeba jukumu la kulipa madeni ya benki hizo. Lakini madeni haya yataweza tu kulipwa iwapo Iceland itachukua mikopo kwa kuwa bajeti ya nchi haiwezi kugharamia. Kwa kulinganisha, kiwango jumla cha fedha za benki hizo tatu ni mara kumi zaidi kuliko pato jumla la taifa linalofikia takriban yuro bilioni 10. Huyu hapa Christoph Ohler, mwanasheria wa maswala ya kiuchumi.

"Tunazungumzia kwa hivyo hali jumla ya uchumi wa Iceland ambapo mapato yanayotokana na kodi hayaleti tija na hivyo kuifanya nchi hiyo kutegemea misaada kutoka nje."

Tangu kuanza mgorogoro wa kiuchumi, shirika la Moody´s limekuwa likishusha juhudi za Iceland kulipa madeni yake, sasa imefikia ngazi nne chini ya kiwango cha maksi kinachoelezwa kuwa kizuri. Hali hii mara moja imesababisha athari katika masoko ya fedha, anasema Alexander Kockerbeck, mchambuzi wa shirika la Moody´s.

"Nchini Iceland viwango vya riba vimeongezeka kwa asilimia kubwa, kwa sababu wakati huu wa mporomoko mkubwa wa kiuchumi unaoikabili dunia, wawekezaji hawataki kuwekeza nchini humo."

Iceland inakabiliwa pia na tatizo la sarafu. Sarafu yake ya Krona imepoteza takriban asilimia 75 ya thamani yake katika miezi iliyopita. Hali hii imekuwa mzigo mkubwa kwa wananchi wa kisiwa hicho, kwa kuwa karibu kila kitu kinachotumika katika maisha ya kila siku huagizwa kutoka nchi za kigeni na hivyo gharama imepanda.