1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AU iko tayari kusimamia utatuzi wa mgogoro Gabon

6 Septemba 2016

Kwa upande mwingine Ufaransa inaishinikiza serikali ya Gabon ikubali mchakato wa kurudiwa tena hatua ya kuhesabiwa upya kura ili kuutatua mgogoro huo uliosababisha vurugu katika taifa hilo

https://p.dw.com/p/1Jwgc
Wafuasi wa Ali Bongo aliyechaguliwa tena madarakani
Wafuasi wa Ali Bongo aliyechaguliwa tena madarakaniPicha: Getty Images/AFP/M. Longari

((Mgogoro wa kisiasa unaendelea nchini Gabon baada ya matokeo ya uchaguzi yenye utata.Waziri wa sheria amejiuzulu kufuatia hatua ya serikali ya kushikilia kukataa kuhesabu upya kura katika matokeo ambayo yamesababisha vurugugu mbaya na hali ya mshike mshike pamoja na madai kwamba ulifanyike wizi na mizengwe katika uchaguzi huo baada ya Rais Ali Bongo kuchaguliwa kurudi tena madarakani. Kuna masuli ya kutosha kuhusu matokeo ya uchaguzi huo yanayoweka msingi wa kuwepo ulazima wa kuhesabiwa tena kura hizo amesema waziri mkuu wa Ufaransa hii leo.

Matokeo yaliyomrudisha tena rais Ali Bongo katika utawala ambao umekuwa ukishikiliwa na familia hiyo kwa takriban miaka 49 yanazua masuali mengi na majibu yake yanaweza tu kuumaliza mgogoro huo kwa kura kuhesabiwa tena kwa mara ya pili, hiyo ndiyo kauli aliyoitowa waziri mkuu wa Ufaransa Manuel Valls hii leo.Waangalizi wa Umoja wa Ulaya walioko nchini Gabon wamekosoa uchaguzi na utangazaji wa matokeo hao kwa misingi ya kuangalia hali halisi bila kupendelea upande wowote ameongeza kusema Valls wakati akizungumza na redio ya Ufaransa ya RTL.Kiasi raia 15 wa Ufaransa hawajulikani waliko nchini Gabon wengi wakiwa wana uraia wa nchi mbili.

Bunge la Gabon likiteketea agosti 31
Bunge la Gabon likiteketea agosti 31Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

Ufaransa, Umoja wa Ulaya pamoja na Marekani zilishatangaza wiki iliyopita kuitaka tume ya uchaguzi ya Gabon ichapishe kikamilifu matokeo ya vituo vyote vya kupiga kura na waziri wa sheria aliyejiuzulu Moundaunga Seraphin ameunga mkono mapendekezo hayo ya jumuiya ya kimataifa ya kura kuhesabiwa upya akisema kwamba kutofanyika mchakato wa kuhesabiwa upya kura huenda ikawa chachu ya kuwasukuma wananchi kuelekea kuchukua hatua za kutumia nguvu kuipinga serikali

Waziri huyo wa sheria aliyejiuzulu jana ameonya kwamba amani na usalama wa nchi yake unakabiliwa na kitisho kikubwa. Serikali ya Gabon imeipuuza miito ya upinzani na nchi za magharibi ya kutaka kura zihesabiwe upya.Bunge la nchi hiyo linatazamiwa kuanza vikao vyake huku wabunge wakijiandaa kukusanyika katika majengo ya baraza la seneti baada ya jengo la bunge la taifa kutiwa moto na kuharibiwa vibaya wakati wa vurugu za maandamano wiki iliyopita.

Umoja wa Afrika kwa upande mwingine umetaarifu kwamba utatuma ujumbe wake kusaidia kuutafutia ufumbuzi mkwamo huo wa kisiasa. Msemaji wa Umoja huo, Jacob Enoh Eben amesema rais Idriss Deby wa Chad ambaye ndiye mwenyekiti wa sasa wa tasisi hiyo ametajwa kuwa tayari kuongoza mazungumzo juu ya Gabon.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Mohammed Khelef