1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AU kuchaguwa mwenyekiti mpya

Admin.WagnerD5 Februari 2012

Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) wanapiga kura zao leo mjini Addis Ababa kumchagua Mwenyekiti wa Kamisheni ya umoja huo, wadhifa muhimu katika uendeshaji wa masuala ya bara la Afrika.

https://p.dw.com/p/13srs
Viongozi wa Nchi za Kiafrika katika mkutano wa 18 wa AU
Viongozi wa Nchi za Kiafrika katika mkutano wa 18 wa AUPicha: picture-alliance/dpa

Nafasi hiyo inagombewa na watu wawili, ambao ni mwenyekiti wa sasa Jean Ping kutoka Gabon na Nkosazana Dlamini Zuma wa Afrika ya Kusini. Hii ni siku ya pili ya mkutano wa 18 wa wakuu wa nchi 54 wanachama wa Umoja wa Afrika, AU. Kwenye siku ya kwanza ya mkutano viongozi hao walimchagua Rais wa Benin Thomas Boni Yayi kuwa mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika  wadhifa ambao ni wakupokezana.

Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ni muhimu zaidi kwa vile mtu atakayechaguliwa atakuwa na majukumu makubwa ya uendeshaji wa umoja huo, ikiwa ni pamoja na kushughulikia usuluhishi wa migogoro inayozikumba nchi kadhaa za bara la Afrika, kama vile Sudan mbili na Somalia.

Mwenyekiti wa sasa wa Kamisheni ya AU, Jean Ping ambaye anagombea mhula mwingine
Mwenyekiti wa sasa wa Kamisheni ya AU, Jean Ping ambaye anagombea mhula mwinginePicha: Reuters

 Wagombea wawili wa nafasi hiyo wote wameelezea matumaini ya Kushinda.  Wa kwanza ni wenyekiti wa sasa Jean Ping kutoka Gabon ambaye vyanzo kutoka kampeni yake vimeelezea matumaini ya uungwaji mkono kutoka nchi zinazotumia lugha ya kifaransa za Afrika ya magharibi na Afrika ya kati. Upande wa Nkosazana Dlamini Zuma, waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje wa Afrika Kusini na ambaye alikuwa mke wa rais wa nchi hiyo Jacob Zuma nao umesema unaamini mgombea wao atashinda.

Mgombea mwingine; Nkosazana Dlamini Zuma kutoka Afrika Kusini
Mgombea mwingine; Nkosazana Dlamini Zuma kutoka Afrika KusiniPicha: picture-alliance/ dpa

Mgombea wa nafasi hii anahitaji kupata theluthi mbili ya kura ambazo zinapigwa kwa siri na wakuu wa nchi au wawakilishi wao, ambao mara nyingi huwa ni mawaziri wa masuala ya nchi za nje. Kura hiyo, kwa mujibu wa taarifa kutoka Addis Ababa, itapigwa saa za mchana leo.

Masuala ya mizozo barani Afrika ilikuwa agenda muhimu kwenye mkutano huu wa wakuu wa nchi  za AU. Akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon aliwatolea wito marais wa Sudan na Sudan Kusini kumaliza tofauti zao juu ya mipaka na biashara ya mafuta kwa njia ya mazungumzo.

Mkutano huu unafanyika katika jengo jipya ambalo lilijengwa na China kwa gharama ya dola milioni mia mbili, na kutolewa kama zawadi kwa Umoja wa Afrika. Rais wa Ethiopia Meres Zenawi amesema sura ya Afrika imekuwa ikibadilika kutoka ile ya mizozo na umasikini, na kuna ishara ya matumaini ya ustawi barani humo.

Viongozi wa AU wanajadili mkakati wa kuongeza biashara baina ya nchi za kiafrika
Viongozi wa AU wanajadili mkakati wa kuongeza biashara baina ya nchi za kiafrikaPicha: picture-alliance/dpa

''Tuna matumaini makubwa kwa siku zijazo, kwa mwongo mzima sasa uchumi wa bara hili umekuwa ukipanda kwa kiwango cha kuridhisha'', amesema Ras Zenawi. ''Tumeweza kuishughulikia na kuisuluhisha migogoro iliyokuwa ikilikumba bara letu, na uwezo wa kufanya hivyo unaongezeka. Utawala bora unashika mizizi taratibu, na ndoto yetu ya kuona Afrika mpya inaanza kutimia.''

Suala jingine muhimu ambalo viongozi wa nchi wanachama wa AU watalishughulikia katika mkutano huu, ni namna ya kuendeleza biashara miongoni mwao, kinyume na sasa ambapo biashara kubwa ni kati ya Afrika na nchi za magharibi na China.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu