1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AU yapata mafanikio nchini Somalia

3 Machi 2012

Vikosi vya Umoja wa Afrika na vile vya Serikali ya Mpito ya Somalia vilichukua udhibiti wa kambi moja ya wanamgambo wa al-Shabaab Kaskazini mwa mji mkuu Mogadishu Ijumaa (02.03.2012).

https://p.dw.com/p/14EKz
Mwanajeshi wa Uganda aweka doria mjini Mogadishu
Mwanajeshi wa Uganda aweka doria mjini MogadishuPicha: AP

Umoja wa Afrika umesema hatua hiyo itapunguza uwezo wa waasi hao kufanya mashambulizi mjini humo. Kutwaliwa kambi ya mafunzo ya Maslah kuna maana kuwa Ujumbe wa Umoja wa Afrika –AU nchini Somalia – AMISOM na Serikali ya Mpito ya Somalia sasa wanadhibiti barabara kuu inayounganisha Mogadishu na maeneo ya kati mwa Somalia.

Serikali tayari imeiteka barabara kuu inayotoka mji mkuu Mogadishu hadi miji ya Kusini mwa nchi hiyo. Taarifa ya AMISOM imesema katika operesheni hiyo iliyoanza jana asubuhi, kikosi cha Uganda kilisaidia kuuteka mji wa Maslah ambao wanamgambo wamekuwa wakiutumia kama kambi yao ya kufanya mashambulizi dhidi ya mji mkuu Mogadishu.

Kamanda wa jeshi la AMISOM, Meja Jenerali Fred Mugisha amesema operesheni hiyo ilipanua ulinzi wa mji huo na itawanyima magaidi hao ngome muhimu ambayo wamekuwa wakiitumia kuwashambulia wananchi.

Raia watano waliuwawa

Mratibu wa huduma za magari ya kuwabebea wagonjwa mjini Mogadishu Ali Musa amesema takribani raia watano waliuwawa, baadhi yao watoto, na wengine kumi wakajeruhiwa katika ufyatulianaji huo wa risasi. Alisema ana uhakika kwamba idadi ya vifo iko juu, kwa sababu hawajafikia maeneo yote ya Kaskazini mwa Mogadishu. Aliongeza kuwa magari yao mengi yalikwama na mashambulizi hayo yalikuwa makali zaidi.

Vikosi vya AU vinaisaidia serikali ya mpito ya Somalia kupambana na wanamgambo
Vikosi vya AU vinaisaidia serikali ya mpito ya Somalia kupambana na wanamgamboPicha: AP

Msemaji wa AMISOM Luteni Kanali Paddy Ankunda, aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa wanajeshi wawili wa Uganda pia walijeruhiwa katika mapambano hayo.

Waasi wa al-Shabaab, kundi ambalo lina mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda, na ambao wanataka kulazimisha uongozi wa kuzingatia kanuni za sharia katika taifa hilo la upembe wa Afrika, wamekuwa katika kampeni ya miaka mitano ya kuiondoa madarakani serikali dhaifu ya Somalia.

Ujumbe wa AMISOM kupanuliwa

Serikali hiyo ya mpito inayoyumba ambayo inaungwa mkono na mataifa ya magharibi, inasaidiwa na takribani wanajeshi 9,000 wa Umoja wa Afrika – AU kutoka Uganda na Burundi na sasa inadhibiti sehemu kubwa ya mji wa pwani wa Mogadishu. Wiki iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepiga kura ya kuupanua ujumbe wa AMISOM hadi karibu wanajeshi 18,000.

Serikali ya Mpito ya Somalia inapambana kuondoa al-Shabaab katika mji mkuu Mogadishu
Serikali ya Mpito ya Somalia inapambana kuondoa al-Shabaab katika mji mkuu MogadishuPicha: picture-alliance/dpa

Al-Shabaab wanapambana na wanajeshi wa Kenya na Ethiopia katika kuchukua udhibiti wa maeneo ya Kusini mwa Somalia na dhidi ya vikosi vya AU karibu na mji mkuu. Vikosi vya Ethiopia na serikali ya Somalia viliukomboa mji muhimu wa Baidoa kutoka mikononi mwa al-Shabaab wiki iliyopita.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters

Mhariri: Sekione Kitojo