1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Augsburg yapata ushindi wa kwanza Bundesliga

4 Novemba 2013

Augsburg walijizatiti ili kuwazaba Mainz mabao mawili kwa moja ikiwa ni ushindi wao wa kwanza msimu huu katika mechi sita. Nayo Bayer Leverkusen iliduwazwa na Eintracht Braunschweig

https://p.dw.com/p/1ABNV
Picha: picture-alliance/dpa

Kocha wa Augsburg Markus Weinzierl alisema baada ya mechi "Kama tu ilivyo katika kila mechi, tulipigana kweli kweli na kupata nafasi. Nadhani hicho kinaonyesha tofauti yetu na pia hatukukata tamaa. Tulicheza mechi tano bila kushinda lakini tulikuwa na ari nzuri katika timu. Nadhani tunaweza kujivunia."

Andre Hahn alitikisa wavu mara mbili wakati Augsburg ikipanda kutoka eneo la kushushwa daraja na kutoshana na Mainz kwa pointi 13. Katika mechi nyingine ya jana, Sergio Garcia alifunga goli katika dakika za mwisho na kuisaidia Werder Bremen kutoka nyuma na kuwashinda Hannover mabao matatu kwa mawili. Ushindi huo umewaweka Bremen katika nafasi ya nane na pointi 15, ikiwa ni mbili mbele ya Hannover ambao wamepata pointi moja tu kutokana na mechi zao tano za mwisho.

Thomas Eichin ni mkurugenzi mkuu wa Werder Bremen "Nilikuwa na imani na timu, ambayo imefanya vyema. Ulikuwa mchezo mzuri wa Bundesliga baina ya timu mbili. Ulikuwa mchuano mzuri kuutazama na nina furaha kuwa tumeweza kuwapa mashabiki ushindi wa nyumbani. Na sasa tunaangazia mechi zijazo tukiwa na utulivu"

Wachezaji wa Werder Bremen wakisheherekea ushindi wao dhidi ya Hannover 98
Wachezaji wa Werder Bremen wakisheherekea ushindi wao dhidi ya Hannover 98Picha: Getty Images

Jumamosi, Bayern Munich walitokwa jasho katika ushindi wao wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Hoffenheim ili kusalia kileleni mwa ligi pointi moja mbele ya Borussia Dortmund ambao siku ya Ijumaa waliwachabanga Stuttgart magoli sita kwa moja. Kocha wa Hoffenheim Markus Gisdol alikuwa na haya ya kusema baada ya mechi "kuna mchanganyiko wa hisia, kwa sababu tulikuwa na mchezo mzuri lakini kwa bahati mbaya mwishowe hatukupata hata pointi."

Bayer Leverkusen wanasalia katika nafasi ya tatu na tofauti ya pointi tatu nyuma ya Dortmund baada ya kuduwazwa Jumamosi kwa kufungwa bao moja bila jawabu na washika mkia Eintracht Braunschweig.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu