1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Austria na Ujerumani zafungua mipaka

6 Septemba 2015

Austria na Ujerumani zimefungua mipaka yao jana Jumamosi(05.09.2015)kwa maelfu ya wahamiaji kutoka mashariki, waliofika kwa mabasi katika mipaka yao wakisafirishwa na serikali ya mrengo wa kulia ya Hungary.

https://p.dw.com/p/1GRkb
Ungarn Flüchtlinge nähe Budapest
Wahamiaji karibu na mji wa Budapest nchini HungaryPicha: picture-alliance/dpa/B. Mohai

Serikali ya Hungary, ilijaribu kuwazuwia wahamiaji hao, lakini wakaelemewa kutokana na idadi yao kubwa.

Wakiachwa kutembea kwa miguu katika kipande cha mwisho cha safari yao kuingia Austria, wahamiaji waliokuwa wamelowa kwa mvua - wengi wa wakimbizi wakiwa ni kutoka katika vita nchini Syria - walisafirishwa kwa treni na mabasi kwenda Vienna na kisha baadaye kupelekwa mjini Munich kwa treni pamoja na miji mingine nchini Ujerumani.

Deutschland Flüchtlinge Bahnhof München
Wahamiaji wakiwasili katika kituo cha treni mjini MunichPicha: Getty Images/A. Beier

Treni ya mwisho iliyobeba wakimbizi wanaokadiriwa kufikia 1,000 iliwasili mjini Munich kutoka Austria asubuhi leo, Jumapili(06.09.2015), na kufikisha idadi jumla ya waliowasili katika mji mkuu wa jimbo la Bavaria tangu Jumamosi kufikia wahamiaji 8,000.

Polisi mara moja waliwaelekeza watu hao kuingia katika treni inayoelekea Dortmund katika eneo lingine la kituo hicho cha treni, lililotengwa kutoka kwa watu waliokuwa wakishuhudia katika kituo kikuu cha treni.

Baadhi ambao walitaka kubakia mjini Munich, awali walikataa kuingia katika treni ya pili, ambayo hatimaye iliondoa na wasafiri wote saa moja baadaye.

Deutschland Flüchtlinge Bahnhof München
Watu waliofika kuwalaki wahamiaji mjini MunichPicha: Getty Images/A. Beier

Wakimbizi wapata mapokezi ya kufariji Munich

Wengi wa wale waliowasili siku ya Jumamosi waliingizwa katika mabasi kwenda katika vituo vya mapokezi ndani na nje ya mji wa Munich baada ya kuchunguzwa afya zao, kupewa chakula na nguo mpya. Wengi wamesema wanatoka nchini Syria, wakati wengine walikuwa ni kutoka Afghanistan ama Iraq.

Walionekana kufarijika mno kusikia sauti za "karibuni Munich," kutoka kwa watu kadhaa waliojitokeza kuwakaribisha ambao walibakia hapo hadi usiku wa manane, pamoja na nia yao ya kuwapatia chokoleti, ndizi ama mikate.

Idadi kama hiyo inatarajiwa kuwasili mjini Munich baadaye leo Jumapili,(06.09.2015).

Deutschland Ankunft Flüchtlinge in München
Wahamiaji wakiwa mjini MunichPicha: Reuters/L. Barth

Wakati huo huo mgawanyiko mkubwa kuhusiana na jinsi ya kushughulikia wimbi la wahamiaji kutoka mashariki ya kati, Afrika na Asia unaleta kitisho kwa maadili ya Umoja wa Ulaya na dunia kwa jumla na huenda ukapunguza uwezo wake wa kuchukua hatua kwa pamoja kuleta mabadiliko katika eneo la mataifa wanachama wa sarafu ya euro na kupunguza matatizo ya madeni nchini Ugiriki.

Wakati zikionekana picha za kusikitisha za watoto waliokufa maji, wakimbizi wakipanda na kushuka kwenye matreni na wakipigwa na polisi, wakizungushiwa waya katika bara la Ulaya, mzozo wa wahamiaji ni sawa na mzozo wa kiroho wa eneo la euro. Katika mikasa yote, msingi wa mshikamano umo katika mtihani mkubwa.

Kwa kuufanya Umoja wa Ulaya kuonekana hauchukui hatua , hauna umoja na bila huruma, mataifa wanachama yakigongana na kuchochea siasa za kujinufaisha pamoja na chuki dhidi ya Waislamu, mzozo wa sasa unakandamiza maadili ya ujumuisho katika Ulaya.

Flüchtlinge am Wiener Bahnhof
Wahamiaji wakiwa mjini Vienna AustriaPicha: Reuters/L. Foeger

Ni mzozo mkubwa kwa Ulaya

Hata hivyo , mara kadhaa inafikia hadi kuingia katika mtafaruku na mivutano kabla ya Umoja wa Ulaya kufikia jibu la pamoja kwa changamoto mpya. Sera huenda zikabadilika kuhusiana na picha ambazo hazivumiliki za mateso, na hofu kwamba kanda ya mataifa ya mkataba wa Schengen ya usafiri bila mipaka miongoni mwa nchi 26 za Ulaya bara huenda ikaporomoka.

Bundeskanzlerin Angela Merkel bei einer Wahlkampfveranstaltung in Essen
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa

"Dunia inatuangalia," kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema wiki iliyopita wakati akijaribu kuwashawishi wenzake wa Ulaya kugawana mzigo kwa kuwachukua watu wanaokimbia vita na maadhila mengine nchini Syria, Iraq, Afghanistan, Libya na kwingineko.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre

Mhariri: Sudi Mnette