1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Avigdor Lieberman ziarani bara ulaya

Jane Nyingi/ AFPE..Picha AFP4 Mei 2009

Waziri wa mambo ya nje wa Israel aelezea umuhimu wa kuiamrishwa uhusiano kati ya Israel na Umoja wa ulaya.

https://p.dw.com/p/HjkE
Waziri wa mambo ya nje wa Israel Avigdor Lieberman.Picha: AP

Waziri wa mambo ya nje wa Israel, Avigdor Lieberman, ameanza ziara yake ya kwanza rasmi barani Ulaya tangu kuingia madarakani. Hii leo Liberman alikuwa nchini Italia na alikutana na waziri mwenzake, Franco Frattini, ambapo aliezea umuhimu wa kuimarishwa uhusiano kati ya Israel na Umoja wa Ulaya.


Mvutano umekuwa ukitokota kati ya Umoja wa Ulaya na Israel, tangu kamishna wa uhusiano wa nje wa Umoja huo, Benita Ferrero-Waldner, kutishia mwezi uliopita kuwa mpango ulionuia kuinua kiwango cha uhusiano kati ya Umoja wa ulaya na Israel hautatekelezwa hadi serikali ya Israel ionyeshe kujitolea kwake katika mashauri ya amani na Palestina.


Liberman anafahamika kwa kauli zake zenye utata na wakosoaji wamekuwa wakimuita mbaguzi kwa matamshi yake dhidi ya watu wenye asili ya kiarabu. Waziri Lieberman amekuwa akisema tatizo kubwa katika eneo la Mashariki ya Kati ni nchi ya Iran, ambayo imeendelea na mpango wake wa kinyuklia, hali inayoyumbisha eneo hilo na ulimwengu mzima.


Bw Liberman alijikuta matatani hivi karibuni baada ya kusema kuwa baraza jipya la mawaziri nchini Israel halijafungamanishwa na maamuzi yaliyoafikiwa na serikali ya hapo kabla katika mkutano wa Annapolisi, Marekani, mwezi November mwaka 2007, kuanza upya majadiliano na Wapalestina.


Waziri huyo machachari anafanya ziara yake ya kwanza barani ulaya tangu aingie madarakani mwishoni mwa mwezi wa Mei mwaka huu. Lieberman pia anatarajiwa kuzuru Ufaransa, Ujerumani na jamuhuri ya Cheki ambayo hivi sasa inashikilia urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya. Ziara hii inawadia wakati uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na Israel ni tete. Umoja huo unataka serikali mpya ya Israel iidhinishe kuwepo dola mbili, dola la Israel na dola la Palestina, ili kutatua mgogoro wa muda mrefu kati yao.


Hata hivyo, waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, hadi kufikia sasa amekataa kuidhinisha kuwepo dola la Palestina kama inavyopendekezwa na mataifa kadhaa ikiwemo, Marekani. Netanyahu anasisitiza uchumi wa Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan unapaswa kuimarishwa kabla ya majadiliano yoyote au maswali mengine.


Waziri huyo mkuu anatarajiwa kuwasilisha sera za serikali yake katika mkutano na rais wa Marekani, Barack Obama, unaotarajiwa kufanyika mjini Washington, Marekani, tarehe 18 mwezi huu.


Wiki iliyopita Israel iliuonya Umoja wa Ulaya dhidi ya kulikosoa baraza la mawaziri la Netanyahu, la sivyo litapoteza jukumu lake kama mpatanishi katika mpango wa amani uliofufuliwa mwezi Novemba mwaka 2007, na ambao umekuwa katika hali mbaya tangu uvamizi wa Isarel katika ukanda wa Gaza mapema mwaka huu.


Afisa mmoja wa Israel alisema onyo hilo lilitolewa wakati wa mazungumzo ya simu kati ya naibu mkurugenzi wa wizara ya mambo ya nje wa Israel katika kitengo cha maswala ya mataifa ya Ulaya Rafi Barak na mabalozi kutoka Uingereza, Ufaransa na Ujerumani.


Rais wa Israel Shimon Peres pia amewatuma nchini Marekani marafiki wake wa karibu wa Israel ili kutuliza hali. Ujumbe wake kwa utawala wa Obama, Israel bado inaamini kuwepo kwa amani.