1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ayatollah: Mousavi wasilisha malalamishi yako katika misingi ya kisheria.

15 Juni 2009

Kiongozi wa juu wa Iran, Ayatollah Khamenei amemtaka Mir Hosein Mosavi- aliyeshindwa katika uchaguzi wa rais kuwasilisha malalamiko yake katika misingi ya kisheria.

https://p.dw.com/p/I9vi
Ayatollah Ali Khamenei, kiongozi wa juu nchini Iran.Picha: AP

Matamshi hayo ya Khamenei, yanakuja wakati serikali ya Iran imeyapiga marufuku maandamano yaliyopangwa kufanywa na wafuasi wa Mir Hossein Mousavi kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyomrejesha madarakani Rais Mahmoud Ahmedinejad.


Anhänger von Mir Hossein Mousavi
Wafuasi wa Mousavi wamekuwa wakiandamana Tehran.Picha: AP

Kwa siku ya tatu mji wa Tehran umegeuzwa uwanja wa vita kati ya polisi wa kupamabana na vurugu na wafuasi wa Mir Houssein Mousavi. Mousavi, aliyeshindwa katika uchaguzi wa rais, amekatalia mbali ushindi wa rais Ahmedinejad, akisema kulikuwa na udanganyifu.


Mousavi sasa ametoa malalamiko yake rasmi katika barua kwa baraza kuu linalosimamia katiba nchini Iran. Mousavi ambaye aliendesha kampeni kama mwanamageuzi, amelitaka baraza hilo lifutile mbali matokeo ya uchaguzi kwa sababu yalikuwa na walakin. Hata hivyo, hata kabla ya wino wa Mousavi kukauka, wizara ya ndani nchini Iran iliokuwa na jukumu la kusimamia uchaguzi ililikataa ombi la Mousavi. Rais Ahmedinejad pia alikatalia mbali kubatilishwa ushindi wake.


Combobild Mahmoud Ahmadinejad und Hossein Mousavi
Rais Ahmedinejad na Mir Houssein Mousavi.Picha: picture alliance / abaca / dpa

Maandamano dhidi ya ushindi wa Ahmedinejad yametawala jiji la Tehran tangu matokeo ya kura kutangazwa. Jumuiya ya kimataifa iliyokuwa ikiyaangalia kwa makini matokeo hayo zimeelezea shaka shaka zao kuhusiana na ushindi wa Ahmedinejad. Makamu wa rais wa Marekani, Joe Biden, alielezea msimamo wa Marekani hadi sasa.


'' inaonekana jinsi wanavyobinya watu wasiseme hadharani, namna wanavyokabiliana na maandamano, inaonekana kuna walakin'' Alisema Biden.

Biden, lakini, alikuwa mwepesi wa kusema Marekani , kama ilivyokuwa kabla ya uchaguzi, itaendelea kuishawishi Iran iachane na mradi wake wa kinuklia.

Umoja wa Ulaya nayo umeitaka serikali ya Iran isitumie nguvu kukabiliana na waandamanaji- ila ichunguze kwa makini madai ya kwamba kura ziliibiwa.


Pigo jingine kwa wafuasi wa Mousavi ni kwamba wizara ya mambo ya nje imepiga marufuku maandamano yaliyopangwa kufanyika leo, kuunga mkono msimamo wa Mousavi kwamba matokeo ya kura yatupiliwe mbali. Wizara ya mambo ya ndani katika taarifa yake ilisema maandamano yeyote yatakuwa kinyume cha sheria, na kwamba yeyote atakayethubutu kuhatarisha usalama wa umma atachukuliwa hatua kali.


Na kama kuonyesha hata nao walikuwa na sauti, mamia ya maelfu ya wafuasi wa Rais Ahmedinejad jana walijitokeza kusherehekea ushindi wake mjini Tehran


Rais Ahmedinejad alitetea ushindi wake akisema daima Iran hufuata misingi ya haki- Ayatollah Khamenei naye amemtaka Mousavi afuate sheria iwapo ana malalamishi yeyote.


Kulingana na kituo cha televisheni cha kitaifa nchini Iran, Rais Mahmoud Ahmedinejad aliyetazamiwa kuelekea leo mjini Moscow kwa mkutano- inasemekana amehairisha ziara hiyo kwa muda kutokana na hali ilivyo nchi Iran.



Mwandishi: Munira Muhammad/ AFP


Mhariri: Miraji Othman