1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Azimio dhidi ya Iran kutojumuisha vikwazo vya silaha.

Sekione Kitojo10 Machi 2007

Wakati baraza la usalama la umoja wa mataifa linaamua kuiadhibu nchi mwanachama , iwe Somalia, Sierra Leone, Liberia ama Iraq, moja kati ya uwezo wake mkubwa unaoenziwa ni madaraka ya kuweka vikwazo jumla vya kijeshi na kudhoofisha huduma za kijeshi za nchi hiyo. Lakini azimio linalodhaminiwa na mataifa ya magharibi katika baraza la usalama ambalo limo katika majadiliano hivi sasa dhidi ya Iran kutokana na urutubishaji wake wa madini ya Uranium , halionekani kuwa litajumuisha vikwazo vya kijeshi kutokana na upinzani kutoka Russia na kwa kiwango kidogo kutoka China.

https://p.dw.com/p/CHIS

Sababu ni kwamba , shirikisho la Russia , ambalo linakura ya veto kama Marekani, Ufaransa, Uingereza na China , ni moja mmoja kati ya nchi zinazoiuzia silaha Iran na ni biashara inayofikia mabilioni ya dola.

Vikwazo vya silaha havitarajiwi , anasema mwanadiplomasia mmoja wa Kiarabu, ambaye haraka anaongeza kuwa , kama vile Marekani inavyolinda uhusiano wake wa kisiasa na kijeshi na Israel, Russia nayo inalinda uhusiano wake wa kiuchumi na kijeshi na Iran.

Iwapo utajaribu kuweka vikwazo vya kijeshi dhidi ya Israel, Marekani itatumia kura yake ya Veto, na iwapo utajaribu kufanya hivyo hivyo dhidi ya Iran , Warusi watatumia kura yao ya turufu.

Mambo ya kiuchumi katika azimio hilo linalopendekezwa yako juu kabisa. Nicholas Burns , afisa mwandamizi katika wizara ya mambo ya kigeni na mmoja kati ya wajumbe wa majadiliano katika muswada wa azimio hilo, alinukuliwa akisema kuwa hakutakuwa pia na vikwazo dhidi ya biashara ya mafuta wala gesi.

Kwa mujibu wa shirika la huduma za utafiti la baraza la Congress lenye makao yake mjini Washington CRS, makubaliano ya mauzo ya silaha kati ya Russia na Iran yanafikia kiasi cha dola bilioni mbili katika kipindi cha mwaka 2002-2005.

Mauzo makubwa kabisa ya mwisho, yaliyothibitishwa mwezi Desemba 2005, yanafikia kiasi cha dola bilioni 1.5, anasema Tom Baranauskas, mchambuzi mwandamizi wa masuala ya mashariki ya kati katika shirika la Forecast International la Marekani, mtoaji mkubwa wa huduma za taarifa za siri za mauzo ya silaha nchini Marekani.

Makubaliano hayo yalijumuisha kuboreshwa kwa ndege za kivita za Iran MiG-29 na na ndege za kivita za Su-24, meli za kivita, maboti yendayo mbio, mfumo wa ulinzi wa makombora TOR-MI, pamoja na uboreshaji wa vifaru vya kivita T-72.

Ni katika uboreshaji wa mfumo wa makombora TOR-MI hasa ambao umezusha upinzani kutoka Marekani na Israel, kutokana na sababu za msingi kuwa makombora haya yanalenga katika kulinda maeneo ya kinuklia ya Iran katika eneo la Bushehr, Baranauskas ameliambia shirika la habari la IPS.

Wakati azimio la kwanza la baraza la usalama la umoja wa mataifa dhidi ya Iran lilipopitishwa mwishoni mwa mwaka jana , Marekani ililazimika kufuta mipango yake ya kuweka vikwazo dhidi ya vinu vya kinuklia vya Bushehr kwasababu ya upinzani mkubwa kutoka kwa Russia. Warusi wanaisaidia Iran kujenga kinu hicho cha kinuklia.

Iwapo Marekani ingesisitiza kuweka vikwazo dhidi ya vinu vya kinuklia , Warusi wangelipinga kwa kura ya veto azimio hilo.

Akiulizwa iwapo China na Russia watakubaliana na vikwazo vya silaha dhidi ya Iran , balozi wa Uingereza Emyr Jones Parry alikwepa swali hilo, akisema sitaki katika wakati huu kuingia katika majadiliano ya nini kila mtu anaweza kukubaliana nacho ama hatakubaliana. Lakini haya ndio mambo ambayo tunayazungumzia.

Pia amewaambia waandishi wa habari kuwa azimio jipya litaangalia juu ya kuongeza vikwazo vilivyopo hivi sasa.

Balozi Alexandro Wolff, kaimu mwakilishi wa kudumu wa Marekani katika umoja wa mataifa , amewaambia waandishi wa habari kuwa biashara ya silaha ya Iran ndio inayojadiliwa hivi sasa .

Sitaki kwenda ndani zaidi, amesema , wakati akiulizwa kutoa maelezo zaidi. Mtazamo wetu ni kwamba kutakuwa na upanuzi kupindukia yale tuliyokuwa tukiyafanya kabla.

Majadiliano juu ya vikwazo vipya vinawajumuisha wanachama watano wa kudumu wa baraza la usalama , Marekani, Uingereza, Ufaransa, China na Russia.