1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baada ya Msikiti Mwekundu, matatizo ya Jenerali Musharraf hayajamalizika

13 Julai 2007

Yeye ni mtu mwenye nguvu kabisa katika Pakistan: Pervez Musharraf. Kama mkuu wa majeshi, aliingia madarakani kwa njia ya mapinduzi, na kwa miaka sasa amekuwa kiongozi wa nchi hiyo. Miezi michache kutoka sasa anataka tena kuchaguliwa kuwa rais, kwani hadi sasa hajachaguliwa kihalali.

https://p.dw.com/p/CHAy
Jenerali Perevez Musharraf, mkuu wa Pakistan
Jenerali Perevez Musharraf, mkuu wa PakistanPicha: AP

Kwa upande mwengine, tangu Septemba 11 mwaka 2001 ameonekana na Marekani kama mshirika wao mkubwa katika kupambana na magaidi wa Kiislamu wenye siasa kali kutoka mtandao wa al-Qaida ambao wamerejea katika maeneo ya mpaka wa Pakistan na Afghanistan. Hali hiyo imemfanya Pervez Musharraf awe na maadui wengi wa kisiasa nchini mwake, na jambo hilo limejitokeza zaidi kutokana na mzozo wa karibuni uliozunguka kushambuliwa Msikiti Mwekundi wa mjini Islamabad:

Alizungumza kwa sauti ya kutafakari, katika hotuba alioitoa kwa wananchi hapo juzi kupitia televisheni, siku moja baada ya kumalizika operesheni za kijeshi katika Msikiti Mwekundu wa Islamabad. Ulikuwa si wakati wa kutamba kwa ushindi bali ni wakati wa maombolezi, alisema mtawala huyo wa kijeshi ambaye mara hii alivalia nguo za kiraia:

+Sasa ni wakati ambapo lazima tutafakari tunaelekea wapi. Nini sisi tufanye, kama wananchi wa Pakistan, tujifanyie nini wenyewe, tuifanyie nini nchi yetu na dini yetu.+

Mara hii hakujakuweko majaribio ya kuwasingizia Wamarekani kwa kila kitu, kama vile ilipotokea wakati wa mashambulio ya Marekani ya Septemba 11, 2001. Pervez Musharraf alikiona kwa muda mfupi kitisho cha Marekani cha wakati huo. Lakini mara hii alikuwa na maeneo makali dhidi ya magaidi na namna wanavoitumia vibaya dini. Naye aliweza kuungwa mkono angalau na Wapakistani wengi. Hadi sasa hakujafanywa maandamano makubwa katika miji mikubwa kupinga kitendo hicho cha kijeshi. Mwishowe aliahidi kwamba majeshi ya usalama yatapambana vikali na wenye siasa kali katika mkoa wa mpakani wa Kaskazini Magharibi na pia dhidi ya shule za Koran katika nchi hiyo.

Suala ni : nani anayemuamini bado rais huyu? Waliberali katika Pakistan hawamuamini tena. Wanajuwa kwamba jeshi la Pakistan tangu zama za mdikteta Zia ul-Haq na wakati wa vita vya chini kwa chini dhidi ya Urussi katika Afghanistan limekuwa, kwa maslahi yake, likiwasaidia Waislamu wenye siasa kali wanaoendesha Jihadi.

Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu isioelemea upande wowote huko Pakistan, Asma Jehangir, amesema:

+Mafungamano baina ya jeshi na Mashehe ni makubwa na ya zamani. Baada ya mkasa wa kuvamiwa Msikiti Mwekundi, mashehe walipata risala inayosema: fanyeni kazi yetu na fanyeni nini kile tunachokuambieni, na mambo yatabakia kuwa mazuri. Lakini mkibadili, basi mambo yatakuwa mabaya.+

Kitisho kikubwa kwa Pervez Musharraf hivi sasa ni kutoka kwa jumuiya za kiraia na vyama vya upinzani vya watu wanaojiweza ambavyo vinamlaumu kwamba alimuondosha kazini, tena kwa kumuaibisha, hakimu mkuu wa nchi hiyo, yote ni kutaka yeye awe na hakika ya kuchaguliwa tena kuwa rais katika majira yajayo ya mapukutiko. Kwa miezi sasa kumekuwa kukifanywa maandamano ambayo yaliwavutia watu wengi zaidi kuliko wale waliopinga kuvamiwa Msikiti mwekundu. Katika upande huu, Pervez Musharraf hafaidiki sana katika mapambano yake ya sasa dhidi ya Waisalmu wenye siasa kali. Mwanajeshi huyo haaminiki tena, na japokuwa kuna watu wengine wanaofikiri kwamba kitendo chake cha hivi karibuni kitamfanya apendwe na watu na kumsaidia kuepukana na matatizo yanayomzunguka kutokana hamu yake ya kutaka achaguliwe tena, lakini bado kuna alama kubwa ya kuuliza kama ataambulia chochote.

Bingwa wa masuala ya Pakistan, Husain Haqqani wa kutoka Chuo Kikuu cha Boston, Marekani anasema mtindo aliokuwa anautumia Musharraf hadi sasa wa kuwagonganisha vichwa wapinzani wake, sasa umefanya awe anakalia baina ya viti vyote:

+Jeshi la Pakistan limekwaruzana na makundi yote muhimu katika nchi hiyo. Watu wenye siasa za Kiislamu wanamchukia Jenerali Musharraf, kwa vile wanamuona kama ni mkono mrefu wa Marekani. Pia waliberali, kwa vile wanamuona ni mdikteta. Watu wa mkoa wa Baluchistan wanamchukia pia kwa vile alimuuwa mkuu wao, Nawab Akbar Bugti, na pia Wapashtu wanamchukia kwa vile amelipeleka jeshi katika eneo la kabila hilo.+

Na katika vyombo vya habari vya nje Musharraf hajapata jina zuri hivi karibuni kutokana na mkasa wa Msikiti Mwekundu. Uhariri katika magazeti ya Kijerumani ulimponda, huku yale ya nchi shirika, kama vile Marekani, yalitaka kufanywe uchaguzi huru na kuweko demokrasia zaidi huko Pakistan. Huenda Musharraf akafikia suluhu na waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Bibi Benazir Bhutto, na kuandaa utaratibu wa kugawana naye madaraka.

Lakini haifikiriwi kwamba jenerali huyo anaweza kuzitambua alama zinazochorwa ukutani mbele yake. Yaonekana kana kwamba atan’gan’gania madaraka kufa na kupona, na kwa hivyo hali ya usalama na utulivu katika nchi hiyo vitazidi kuwa katika mbinyo.