1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Netanyahu asema Israel "iko vitani"

Daniel Gakuba
7 Oktoba 2023

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema Israel ''iko vitani'' baada ya kundi la Hamas kuvurumisha maelfu ya makombora ndani ya Israel. Wanamgambo wa kundi hilo la Palestina wamefanikiwa kupenya ndani ya Israel.

https://p.dw.com/p/4XF5o
Wanajeshi wa Israel mjini Sderot
Wanajeshi wa Israel mjini SderotPicha: Ammar Awad/REUTERS

Hamas imetangaza asubuhi ya Jumamosi kuwa imefyatua makombora 5,000 ikilenga shabaha ndani ya Israel. Jeshi la Israel (IDF) limeeleza katika taarifa kuwa ''wapiganaji magaidi'' wamefanikiwa kujipenyeza ndani ya Israel.

Waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant amesema Hamas imefanya ''kosa kubwa sana'' kwa kuanzisha vita hivyo dhidi ya Israel.

Jeshi la Israel limesema kuwa limejibu mashambulizi ya Hamas kwa kuzilenga shabaha kadhaa katika Ukanda wa Gaza.

Umoja wa Ulaya wasema kuwashika mateka raia ni kinyume na sheria ya kimataifa

Mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell, akizungumzia taarifa kuwa raia wa Israel wamechukuliwa mateka na wanamgambo wa Kipalestina, amesema ''rIpoti kwamba raia wametekwa nyara majumbani mwao, au ndani ya Gaza ni za kuchukiza.''

Akiandika katika mitandao ya kijamii, Borrell amesema kitendo hicho ni ''kinyume na sheria ya kimataifa'' na kutaka mateka wote waachiwe mara moja.

Vyombo vya habari vya Israel vimearifu kuwa wanamgambo wa Kipalestina wamewachukuwa mateka raia katika miji kadhaa, na kwamba baadhi wamepelekwa katika Ukanda wa Gaza. Taarifa hizo hazikuweza kuthibitishwa.

Idadi ya Waisraeli waliouawa yafika 40

Kitengo cha Israel cha magari ya kuwabeba wagonjwa kimeripoti kuwa Waisraeli 40 wameuawa katika shambulizi hilo la Hamas, wakiwamo waliouawa kwa maroketi na katika hujuma za ardhini. 

Kikosi cha zimamoto kikiuzima moto uliotokana na mashambulizi
Kikosi cha zimamoto kikiuzima moto uliotokana na mashambulizi Picha: Amir Cohen/REUTERS

Kitengo hicho pia kimesema kuwa kimewapatia matibabu mamia ya wengine waliojeruhiwa. Watu zaidi ya 770 wameripotiwa kupata majeraha.

Ripoti kutoka eneo la mapigano zilizosambaa katika mitandao ya kijamii, zimeeleza kuwa wanamgambo wa Kipalestina wameufikia mji wa Sderot kusini mwa Israel na kuwachukua watu mateka.

Vyombo vya habari vya Israel vimesema kuwa wanamgambo hao walikuwa wakifyatua risasi kiholela kuwalenga wapita njia. Jeshi la Isreal limesema linaelewa kuwepo kwa ripoti za watu kushikwa mateka, bila hata hivyo kutoa maelezo zaidi.

Ujerumani, Umoja wa Ulaya, walaani mashambulizi ya Hamas

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema ameshtushwa na habari zinazotoka ndani ya Israel, na kupitia mitandao ya kijamii amesema Ujerumani inasimama pamoja na Israel.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen pamoja na rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel pia wameelezea mshikamano wao na Israel inapokabiliwa na mashambulizi ya Hamas.

Marekani pia imesema inalaani kwa nguvu zote mashambulizi ya Hamas, na kwamba iko bega kwa bega na serikali ya Israel pamoja na watu wake. Wizara ya Ulinzi mjini Washington imesema itaipa Israel msaada wowote inaouhitaji ili iweze kujilinda.

Kikao cha dharura cha usalama baada ya mashambulizi Israel
Kikao cha dharura cha usalama baada ya mashambulizi IsraelPicha: Haim Zach/GPO/AA/picture alliance

Katika kanda ya Mashariki ya Kati, rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas amesema Wapalestina wanayo haki ya kujilinda dhidi ya ''ugaidi wa walowezi na jeshi linalozikalia kimabavu ardhi zao'', hii ikiwa ni kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la WAFA.

Wizara ya mambo ya nje ya Saudi Arabia imesema nchi hiyo inafuatilia kwa karibu hali ya mambo, na kuzitaka pande zote kuacha ghasia.

Vyanzo: ab/dj (dpa, AFP, AP, Reuters)