1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baada ya Ugiriki na Ureno,je, sasa ni Spain ?

29 Aprili 2010

Hatua za kumaliza msukosuko wa Euro.

https://p.dw.com/p/N9O1
waziri wa fedha wa Spain Elena Salgado (kati-kati)Picha: AP

Msukosuko wa madeni unaliyumbisha bara la ulaya wakati huu:Baada ya Ugiriki na Ureno, kuonekana haziaminiki kupewa mikopo,jiinamizi hilo sasa limeiangukia nchi nyengine ya Umoja wa Ulaya: Uhispania.

Shirika maarufu -Standard & Poor's (S&P)-linalotathmini uwezo wa mkopaji kuhimili madeni , jana uliiteremsha hadhi ya Spain kwa pointi 1. Matumaini ya kustahiki kupewa mikopo kwa hivyo, si mema kwa nchi hiyo.

Wachambuzi nchini Uhispania, wanailaumu Ujerumani, kwa tabia yake ya kusitasita kuiokoa Ugiriki, kama mojawapo ya sababu zilizochangia kushushiwa Uhispania uwezo wake wa kuhimili madeni. Hatua zimekawia kuchukuliwa, asema pia Juan Ignacio Crespo,mkurugenzi wa shirika la habari za kiuchumi -Thomson Reuters:

"Kile kilichoanza kama dharuba ndani ya glasi ya maji, ingewezekana hapo Februari, kukipatia ufumbuzi bila ya taabu kubwa. Kwani Ugiriki pato lake la taifa ni 2 tu % ya pato jumla la nchi zanachama wa Umoja wa Ulaya.Sasa, lakini, imekuwa taabu zaidi kuleta ufumbuzi na mtindo uliofuatwa hadi sasa wa uzembe ukiselelezwa , basi tutakabiliwa na dharuba kali."

SOKO LA HISA

Soko la hisa la Madrid lilipoteza hapo jana kiasi cha 3% na hii baada ya hasara iliopatikana wiki iliotangulia ilipofutwa kiasi. Soko la Hisa la IBEX35 kwa muda wa siku 2 tu lilianguka kwa hadi 4%. Soko hilo la fedha wakati huu ni la wasi wasi kabisa kutokana na matatizo ya dhamana za mikopo iliobeba serikali.Crespo anasema hata hivyo:

"Kuna habari nzuri sana kwa masoko ya hisa na hasa juu ya faida nono za makampuni na pia katika masoko hayo ya hisa ya Uhispania. Na nchini Marekani, matokeo ni hata bora zaidi kuliko ilivyotarajiwa. Lakini, masoko ya mikopo ya Ulaya yote yameyumbishwa."

IMANI KWA SPAIN:

Hata serikali ya Spain, inajitahidi kutuliza mambo. Waziri-mkuu, Zapatero, ameeleza Bungeni kwamba, kuna dalili kwamba uchumi wa Uhispania unaanza kustawi: matumizi ya umeme yanaongezeka, motokaa zaidi zinauzwa na mapato ya kodi yameanza tena kuongezeka. Na baada ya Shirika linalotathmini uwezo wa nchi kukopo kuiteremsha Uhispania, kidogo chini hadhi yake alaasiri ya jana, Makamo waziri mkuu wa nchi hiyo, de la Vega, amewataka wananchi na masoko ya fedha kuwa na imani na Uhispania.Makamo waziri mkuu de la Vega, aliwaambia wananchi na masoko na ninamnukulu,

"Tumepitisha hatua za kuimarisha barabara uchumi ili kasoro iliopo katika bajeti, kuipunguza hadi kima cha 3% ifikapo 2013. Kuna mpango wa kubana matumizi. Tunafanya marekebisho ya soko la kazi na kila juhudi ili kutimiza ahadi tulizotoa."

SERIKALI YA SPAIN

Serikali ya Uhispania, kwa hivyo, inapanga kupunguza matumizi kwa kima cha hadi Euro bilioni 50. Miongoni mwa hatua hizo, ni mageuzi ya bima ya uzeeni-(pensheni ) na kuanzia Julai mosi, kodi ya ununuzi itapanda kutoka kima cha sasa cha 16 % hadi 18%.

Mwandishi: Spiegelhauer,Reinhard

Mtayarishi: Ramadhan Ali

Mhariri: Miraji Othman