1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baada ya ushindi mkubwa, Macron aahidi kuiunganisha Ufaransa

Bruce Amani
8 Mei 2017

Akizungumza mbele ya maelfu ya wafuasi wake usiku wa kuamkia leo, rais mteule Emmanuel Macron amesema kazi kubwa bado inawasubiri akiapa kuitetea Ufaransa, maslahi yake muhimu pamoja na maadili na uhuru wa taifa hilo.

https://p.dw.com/p/2caRP
Frankreich Präsident Emmanuel Macron spricht vor dem Louvre in Paris
Picha: Reuters/B. Tessier

Macron alichaguliwa jana kuwa rais wa Ufaransa baada ya kumshinda Marine Le Pen katika duru ya pili ya uchaguzi.

Wizara ya mambo ya ndani ya Ufaransa ilisema Macron, kiongozi wa siasa za wastani, ameshinda kwa asilimia 66 ya kura.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 39, ana maono ya kuweka mazingira bora ya biashara katika Umoja wa Ulaya kitu ambacho kiliwavutia wapiga kura.

Mpinzani wake wa siasa kali za mrengo wa kulia, Le Pen, alifanya kampeni zake kwa kutishia kuiondoa Ufaransa katika Umoja wa Ulaya. 

Mapema leo, rais huyo mteule wa Ufaransa alizungumza kwa njia ya simu na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, ambapo ameahidi kuizuru Berlin hivi karibuni.

Vile vile, Macron alijadiliana na Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May juu ya suala la Uingereza kujiondoa kwenye Umoja huo.

Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte, ambaye alishinda uchaguzi mwezi Machi dhidi ya wapinzani akiwemo kiongozi wa siasa kali za mrengo wa kulia Geert Wilders, pia amempongeza Emmanuel Macron kufuatia ushindi wake.

Jean Claude Juncker, rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya, amemwambia Macron kuwa ana furaha kuwa mawazo aliyoyatetea ya Ulaya imara na yenye maendeleo, ambayo inawalinda raia wake wote ndiyo atakayoingia nayo madarakani.