1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baba mtakatifu aikosoa Israel kuhusu ardhi ya Wapalestina.

25 Oktoba 2010

Wapalestina wafurahia wazo la Baba mtakatifu, Waisraeli walinyoshea kidole cha lawama.

https://p.dw.com/p/PnHQ
Baba mtakatifu, Benedict wa 16 alisema uhuru wa kuabudu unafaa kuheshimiwa.Picha: AP

Mkutano wa wiki mbili, uliowaleta pamoja maaskofu kutoka eneo la mashariki ya kati, ulilipa kipau mbele suala tete la amani na maridhiano kama njia ya kuwezesha mazungumzo kati ya Waislamu na Wakristu.

Baba mtakatifu Benedict wa 16, akizungumza katika misa ya kuufunga mkutano huo, katika kanisa la mtakatifu Peter kule Vatikani, alisema kupunguka kwa waumini wa kikristu mashariki ya kati kumekuwa jambo la kutia wasiwasi, hasa ikizingatiwa kwamba huko ndiko chimbuko la Ukristu. Alisema kutokota kwa mizozo, ubaguzi na matatizo ya kiuchumi yamechangia pakubwa katika kudhalilisha haki ya raia na ni muhimu haki ya kuabudu iheshimiwe.

Maaskofu kutoka mashariki ya kati waliouhudhuria mkutano huo, walikubaliana kwa pamoja na kutoa nyaraka kuhusu mustakabali wa kanda hiyo. Nyaraka hiyo iliikashifu Israel ikitaja kwamba lazima isitishe harakati zake za unyanyasaji kwa kuendeleza sera za kukalia ardhi ya Wapalestina.

Baba mtakatifu alisema mataifa ya mashariki ya kati yanafaa kuzingatia uhuru wa kuabudu. Kiasi ya Wakristu milioni 3.5 kutoka madhehebu mbalimbali wanaishi katika ghuba ya Arabu. Nchini Saudi Arabia, kwa mfano, waumini wa kikristu huabudu kisiri na Waislamu wanaobadilisha dini wanaweza kutolewa adhabu ya kifo, ingawa hukumu kama hiyo ni nadra kutolewa.

Baba matakatifu Benedict wa 16, akizungumzia suala tete la amani mashariki ya kati, alisema Israel haifai kutumia mistari ya Biblia kuhusu ‘taifa waliloahidiwa au Wayahudi kama watu waliochaguliwa’, ili kutekeleza ujenzi wa makaazi mapya kwa manufaa ya walowezi wa Kiyahudi mjini Jerusalem na Ukanda wa Gaza.

Papst Benedict XVI während der offiziellen Verabschiedungszeremonie in Israel
Baba mtakatifu akiwa na rais wa Israel, Shimon Peres, kulia na Waziri mkuu, Benjamin Netanyahu katika ziara yake ya 2009.Picha: AP

Hoja hiyo imekaripiwa na Israel ikisema kwamba matamshi hayo ni uvamizi wa kisiasa kwa taifa hilo la Kiyahudi.

Naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Israel, Danny Ayalon; amesema kwamba wameghadhabishwa na mtazamo huo. Bw Ayalon alisema haikufaa masuala mazito kama hayo kujadiliwa katika mkutano wa maaskofu ambao walitumia fursa hiyo kuikashifu Israel kwa misingi ya historia na propaganda za Kiarabu. Alisema mkutano huo ulihudhuriwa na washiriki wengi ambao wanaipinga Israel.

Kwa upande wa Wapalestina, wazo hilo limepokelewa kwa uzuri. Mpatanishi wao, Saeb Erekat; alisema Wakristu wanakubalika kati ya Wapalestina na akailaumu Israel kwa kuendeleza ubepari ambao unatishia kuwepo kwa taifa huru la Palestina. Bw Erekat alisema wanaunga mkono mapendekezo yaliyotolewa baada ya mkutano huo wa maaskofu yanayotoa mwito kwa Jumuiya ya kimataifa kuimarisha maadili ya uhuru na haki kwa sababu ina jukumu la kisheria pia kuhakikisha Israel haiendelei kukalia ardhi ya Wapalestina.

Mapendekezo ya maaskofu hao yaliuiana na yale ya Umoja wa Mataifa yanayoitaka Israel iondoke katika ardhi iliyonyakua katika vita vya siku sita mwaka wa 1967. Kwa sasa mwelekeo wa mazungumzo ya amani unaonekana kuyumbayumba, huku Wapalestina wakidai kwamba hawatarejea katika mazungumzo ya amani ikiwa walowezi wa Kiyahudi wataendelea kujenga makaazi yao mashariki mwa mji wa Jerusalem .

Mwandishi: Peter Moss /Reuters/AFP/AP

Mhariri: Othman Miraji.