1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baba mtakatifu awasili Cameroon

Aboubakary Jumaa Liongo/AFP/DPA17 Machi 2009

Baba mtakatifu Benedicto wa 16 amewasili katika mji mkuu wa Cameroon Younde, mwanzoni mwa ziara yake ya mataifa mawili barani Afrika.

https://p.dw.com/p/HEGC
Pope Benedict XVIPicha: AP

Wakati akiwa njiani kuelekea nchini humo, baba mtakatifu alisema kuwa matumizi ya mipira ya kinga yaani kondom siyo suluhisho la kupambana na maradhi ya Ukimwi.


Baba mtakaktifu ambaye hii ni ziara yake ya kwanza katika bara hilo la Afrika lililoathiriwa kwa kiasi kikubwa na maradhi ya ukimwi, amepinga dhahiri dhana kuwa matumizi ya kondomu ni njia mujarabu ya kupambana na kuenea kwa maradhi hayo.


Amesema kuwa ukimwi ni janga ambalo haliwezi kupigwa vita kwa kutumia fedha pekee, kuweza kulishinda kwa kusambaza mipira hiyo ya kiume ambayo amesema zaidi inazidisha kusambaa kwa maradhi hayo.


Suluhisho pekee ambalo baba mtakaktifu amesema kuwa ni uamsho wa kiroho na kimwili miongoni mwa wanajamii pamoja na kuwapenda wale wote waliyoathirika na janga hilo.


Nchi zilizoko kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika zimeathirika kwa kiasi kikubwa na maradhi ya Ukimwi, kuliko eneo lingine lolote duniani.


Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na ukimwi UNAIDS Takriban theluthi mbili ya watu wote wazima na watoto wenye virusi vya HIV duniani wanatoka katika eneo hilo.


Kanisa kwa muda mrefu limejikuta katika msuguano na wanaharakati wa ukimwi kutokana na msimamo wake wa kupinga matumizi ya kondomu pamoja na dawa za kupanga uzazi


Mwaka jana kiasi cha makundi 60 ya kanisa hilo yaliandika barua kwa baba mtakatifu kumtaka abadilishe msimamo wa kanisa kupinga matumizi ya kondomu pamoja na dawa za kupanga uzazi.

Aidha baba mtakatifu ambaye mwezi ujayo anatimiza miaka 82,akizungumza na waandishi wa habari ndani ya ndege yake akiwa njiani kuelekea Cameroon, pia alipiga taarifa kwamba amekuwa mpweke kutokana na mzozo uliyotokana na hatua yake ya kutengua uamuzi wa kumuondoa kundini askofu aliyetangaza kupinga kuwepo kwa mauaji ya wayahudi ya Holocaust,Richard Williamson.


Amesema kuwa dhana kwamba hatua yake hiyo imemfanya awe mpweke humfanya acheke, na kupinga taarifa za vyombo vya habari vya Italia kwamba ametengwa, akisema kuwa amezungukwa na marafiki wengi.


Ziara hiyo ni ya kwanza kwa baba mtakatifu barani Afrika, ambapo amesema anataka kulibariki bara hilo.Mbali ya Cameroon pia anatarajiwa kuitembelea Angola.


Mwezi uliyopita alitangaza kuwa anataka mwaka huu wa 2009 kuwa mwaka wa Afrika utakaojumuisha pia mkutano wa maaskofu wa Afrika mwezi Septemba mwaka huu mjini Roma, pamoja mkutano wa majimbo ya kanisa barani Afrika utakaofanyika Vatican Octoba mwaka huu.


Kiongozi huyo wa katoliki duniani atakuwa nchini Cameroon mpaka Ijumaa wiki hii, ambapo atakutana na wawakilishi wa kanisa hilo kutoka nchi 52 za Afrika wanaofanya maandalizi ya mkutano huo wa majimbo ya kanisa.


Aidha baba mtakatifu mbali ya kuendesha misa ya wazi, pia anatarajiwa kukutana na wawakilishi wa jumuiya ya waislam pamoja na wawakilishi wa vyama vinavyoshughulika na walemavu.

Akiwa nchini Angola, nchi ambayo bado inajaribu kujinasua kutokana katika makovu ya vita vya miaka 27 vya wenyewe kwa wenyewe, baba mtakatifu atakutana na wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi zao nchini humo.