1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baba Mtakatifu Benedict VXI aongoza misa kubwa mjini Nazareth

Charo Josephat14 Mei 2009

Papa Benedict XVI atetea utamaduni wa ndoa kati ya mume na mke

https://p.dw.com/p/HpmW
Papa Benedict XVI akiongoza misa mjini NazarethPicha: AP

Baba Mtakatifu Benedict XVI leo asubuhi ameongoza misa katika mlima wa Precipice, nje kidogo na mji wa Nazareth. Misa hiyo ya mwisho imekuwa kubwa kati ya misa zote alizoongoza wakati wa ziara yake nchini Israel na katika maeneo ya Wapalestina.

Misa hiyo maalum imeanza muda mfupi baada ya Baba Mtakatifu Benedict XVI kuwasili mjini Nazareth kwa helikopta, mji ambako Yesu Kristo aliishi wakati wa ujana wake. "Salam Lakum" Amani iwe kwenu, amewaamkia mahujaji takriban 40,000 waliokuwa wakimshangilia na kupeperusha bendera.

Mmoja wa mahujaji hao amepaza sauti akisema, Viva al-Baba, na kusababisha kelele za shangwe kutoka kwa umati wa watu, hatua ambayo imemfurahisha Baba Mtakatifu na kumuacha akicheka katika eneo hilo la kilima ambapo inaaminiwa Yesu Kristo alipotea wakati umati wa watu waliokuwa wamekasirishwa na mafundisho yake walipojaribu kumsukuma kwenye jabali.

"Hii ni ndoto kumuona papa wetu," amesema Moses Denorio, raia wa Ufilipino ambaye amekuwa akiishi nchini Israel kwa miaka 25 sasa na ambaye ameandamana na mahuaji wenzake kwenye mabasi matatu kuja kumuona Baba Mtakatifu. Moses ameongeza kusema na hapa namnukulu, "Ni kitu muhimu sana kumuona Baba Mtakatifu. Ni baraka kwetu na ni baraka kwa mji wa Nazareti. Tunaombea amani nchini Israel na kwa Wapalestina. Tunaomba bila kupoteza tumaini," mwisho wa kumnukulu.

Papst Benedikt in Nazareth Israel
Papa Benedict XVI akiwasalimia waumini wakati alipokuwa akiwasili kwa misa mjini NazarethPicha: AP

Baba Mtakatifu amesema ulimwengu unahitaji maadili ya jamii na kutetea utamaduni wa ndoa kati ya mume na mke.

Mwito kwa Wakristo na Waislamu

Akiwa mjini Nazareth, mji wenye idadi kubwa ya waarabu na asilimia 30 ya wakazi 66,300 wa mji huo wakiwa Wakristo, Baba Mtakatifu amewahimiza Wakristo na Waislamu kuweka tofauti zao kando na kujenga mahusiano yatakayowawezesha kuishi kwa amani. Amewataka waumini waige mfano ya Yesu Kristo na wazazi wake Mariamu na Yusufu ili wafahamu utakatifu wa familia hiyo.

Mipango ya kujenga msikiti karibu na kanisa la Katoliki mjini Nazareth mnamo mwaka 1999 ilizusha hasira miongoni mwa jamii ya Wakristo na kusababisha hali ya wasiwasi mjini humo. Misingi ya msikiti huo ilijengwa lakini ikavunjwa mnamo mwaka 2003 kufuatia amri ya mahakama ya Israel. Kijana huyu wa Nazareth anasema uhusiano baina ya Wakristo na Waislamu mjini humo ni mzuri na kila mtu anataka kuishi kwa amani.

"Tunashirikiana kwa sababu Wakristo na Waislamu wana hamu ya kufahamiana. Na hata kama kuna mambo fulani ambayo hayakubaliki na upande mmoja, kwa ujumla naweza kusema mambo ni mazuri kati yetu. Watu wanataka kuishi kwa amani na wengine"

Kundi dogo lenye msimamo mkali wa dini ya kiislamu mjini Nazareth limeipinga ziara ya Baba Mtakatifu likiwa bado limekasirishwa na matamshi ya kiongozi huyo aliyoyatoa mwaka 2006 alipomnukulu mfamle wa kikristo aliyesema baadhi ya mafundisho ya mtume Muhammad yalikuwa maovu na yasiyo na ubinadamu.

Papa kukutana na Netanyahu

Papa Benedict VXI anatarajiwa baadaye leo kukutana na maafisa wa kanisa la mjini Nazareth pamoja na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Papst Benedikt in Nazareth Israel
Papa Benedict XVIPicha: AP

Mkutano kati ya Baba Mtakatifu na waziri mkuu Netanyahu, unafanyika siku moja baada ya papa kuutembelea mji wa Bethelemu katika Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan ambako alifanya mazungumzo na rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Mahmoud Abbas.

Mjini Bethlehemu Baba Mtakatifu ametoa mwito kuundwe taifa huru la Wapalestina na kueleza masikitiko yake kuhusu ukuta wa Israel unaotenganisha miji ya Bethlehemu na Jerusalem. Ametaka pia kuzingirwa kwa Ukanda wa Gaza na Israel kumalizike.

Katika ratiba yake ya leo papa Benedict XVI pia amepangiwa kulitembelea kanisa lililojengwa mahala ambapo inaaminiwa malaika Gabrieli alimtokea bikira Mariamu na kumpasha habari kwamba atamzaa mwana Yesu Kristo atakayekuwa mkombozi wa ulimwengu.

Mwandishi: Josephat Charo/AFP/DPAE

Mhariri: Abdul-Rahman